Van Dijk amtwisha lawama Chiesa
Muktasari:
- Kikosi cha Wolves chini ya kocha Rob Edwards kilipata ushindi wa kushtua wa mabao 2-1, huku Liverpool ikikosa nafasi ya kupanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kutokana na kipigo hicho.
LIVERPOOL, ENGLAND: BEKI wa kati na nahodha wa Liverpool, Virgil van Dijk ameelekeza lawama zake kwa Federico Chiesa baada ya bao la ushindi la Wolves katika dakika ya 94 uwanjani Molineux kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa Jumanne usiku.
Kikosi cha Wolves chini ya kocha Rob Edwards kilipata ushindi wa kushtua wa mabao 2-1, huku Liverpool ikikosa nafasi ya kupanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kutokana na kipigo hicho.
Mohamed Salah alifunga bao la kusawazisha dakika ya 83 katika dakika za mwisho zenye msisimko, baada ya Rodrigo Gomes kuifungia Wolves bao la kwanza. Hata hivyo, Andre aliibuka shujaa kwa kufunga bao la ushindi dakika ya 94 na kuzua shangwe kubwa kwa mashabiki.
Nahodha wa Liverpool, Van Dijk, alikasirishwa sana na bao hilo na alipaza sauti kuelekea kwa Chiesa, akionekana kutoridhishwa na mchango wa winga huyo wa Italia. Alisson Becker alikuwa amepiga pasi ndefu kuelekea kwa Chiesa, lakini baada ya wawili hao kushindwa kuunganisha, Chiesa hakurudi haraka kusaidia kuokoa mpira. Shuti la Andre baadaye lilimgonga mchezaji na kumbabatiza Alisson kabla ya kuingia wavuni.
Katika mahojiano baada ya mechi, Van Dijk alionekana mtulivu zaidi, lakini bado alionesha kukerwa na namna walivyofungwa.
“Kufungwa mabao huwa kunakera kila wakati,” aliiambia TNT Sport alipoulizwa kuhusu kufungwa kwao. “Tumetoka kwenye mechi kadhaa bila kuruhusu bao na nadhani kiulinzi tumekuwa imara sana.
“Lakini ndivyo ilivyo, tunapaswa kusonga mbele haraka kwa sababu tutarejea hapa baada ya siku chache na tunataka kufanya vizuri pia kwenye Kombe la FA, hivyo lazima tuonyeshe mwitikio.”