Utovu wa nidhamu wamgharimu Aubameyang, atimuliwa Marseille
Muktasari:
- Nyota huyo wa zamani wa Arsenal, anaripotiwa kumpasulia kizima moto (fire extinguisher) Bob Tahri, ambaye ni mwakilishi wa mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo. Tahri alikuwa kambini hapo kutekeleza amri ya wachezaji kuwahi kulala.
HALI ya sintofahamu inaendelea kuikumba klabu ya Marseille nchini Ufaransa, baada ya mshambuliaji, Pierre-Emerick Aubameyang, kuondolewa kikosini kufuatia utovu wa nidhamu kwenye kambi ya timu hiyo.
Aubameyang (36) anadaiwa kuongoza kundi la wachezaji kumi kufanya sherehe ya ghafla usiku wa Alhamisi iliyopita kwenye kituo cha mazoezi cha Robert Louis-Dreyfus (La Commanderie), ambako wachezaji walikuwa wamewekwa kizuizini kwa lazima ili kurejesha viwango vyao.
Nyota huyo wa zamani wa Arsenal, anaripotiwa kumpasulia kizima moto (fire extinguisher) Bob Tahri, ambaye ni mwakilishi wa mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo. Tahri alikuwa kambini hapo kutekeleza amri ya wachezaji kuwahi kulala.
Mbali na kummwagia Tahri, Aubameyang aliharibu kitanda na vifaa binafsi vya kiongozi huyo. Tahri, ambaye ni mshindi wa zamani wa nishani ya fedha ya mbio za kuruka viunzi na maji duniani, aliripoti kitendo hicho kwa uongozi wa juu wa klabu kwa hasira. Ripoti kutoka Foot Mercato zinaeleza kuwa vyumba vya wachezaji vilitawaliwa na hali ya fujo na uchafu.
Ingawa Aubameyang aliomba radhi akidai alikuwa anajaribu tu ‘kuchangamsha mazingira’, uongozi wa Marseille chini ya kocha Habib Beye umechukua hatua kali kwa kumwondoa mshambuliaji huyo kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Le Havre juzi Jumapili, Mei 10, 2026.
Kambi hiyo ya lazima iliamriwa na mabosi wa klabu kama majibu ya matokeo mabaya ya timu hiyo tangu kuondoka kwa kocha Roberto De Zerbi mwezi Februari aliyekwenda Tottenham. Marseille imeshinda mechi moja tu ya ligi tangu Machi 13, hali iliyopoteza matumaini yao ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya ( UEFA Champions League) na sasa inapambana kusalia nafasi ya saba ili kupata nafasi ya michuano ya Ulaya.
Hata hivyo, amri hiyo ya klabu imekosolewa kisheria. Mwanasheria wa masuala ya kazi jijini Paris, Pierre Vignal, aliiambia RMC kuwa kitendo cha kuwazuia wachezaji kambini kinaweza kutafsiriwa kama unyanyasaji wa kikazi na kuzuia uhuru wa kutembea kinyume na sheria za kazi.
Kando na sakata la Aubameyang, aliyekuwa mshambuliaji wa Manchester United, Mason Greenwood, naye ameingia kwenye dhoruba kali la lawama kutoka kwa mashabiki na vyombo vya habari.
Baada ya Marseille kukubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Nantes inayopambana kutoshuka daraja, Greenwood na wachezaji wenzote walipewa alama sifuri (0/10) na gazeti la ndani la La Provence, huku Greenwood akitafsiriwa kama ‘mwigizaji wa sarakasi’ na uchezaji wake kuitwa wa ‘kihuni’.
Ripoti zinaongeza kuwa, Kocha Habib Beye alilazimika kusimamisha mazoezi mapema wiki hii baada ya Greenwood kukaidi maelekezo. Gazeti la L'Equipe nalo limefichua kuwa mshambuliaji huyo wa England amewakera viongozi kwa mtindo wake wa kukosa vipindi vya kujifunza lugha ya Kifaransa pamoja na kuruka huduma za lazima za matibabu.