Utata waifunika El Clasico Madrid ikijipigia tena Barca

Muktasari:

  • Barca ilidhani kwamba imefunga bao la pili, lakini mpira wa Lamine Yamal uliamriwa na VAR kwamba haukuwa umevuka mstari na jambo hilo limeibua mjadala juu ya kukosekana kwa teknolojia ya mstari wa goli kwenye mikikimikiki ya La Liga.

MADRID, HISPANIA. Jude Bellingham inaonekana ni kama anapenda sasa kucheza dhidi ya Barcelona. Kiungo huyo mpya bado mpya kwenye mechi za El Clasico, lakini tayari ameshaonyesha makali yake katika kipute hicho cha mahasimu wakubwa Hispania.

Jumapili, alicheza mechi yake ya tatu ya El Clasico msimu huu na alifanya jambo kubwa, akifunga bao la ushindi kuisaidia Real Madrid kuichapa Barcelona 3-2 na kukisogeza kikosi hicho cha Carlo Ancelotti karibu na ubingwa wa La Liga msimu huu.

Katika mchezo huo, Barcelona ilianza kuonyesha makali, ikitumia faida ya kuanza hovyo kwa Real Madrid. Barca ilitangulia kwa bao la kona, ambapo kipa Andriy Lunin alifanya makosa kumruhusu Andreas Christensen kufunga kwa kichwa. Lakini, Los Blancos ikaamka, ikifunga bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti ya Vinicius Jr baada ya Pau Cubarsi kumfanyia madhambi Lucas Vazquez ndani ya boksi.

Barca ilidhani kwamba imefunga bao la pili, lakini mpira wa Lamine Yamal uliamriwa na VAR kwamba haukuwa umevuka mstari na jambo hilo limeibua mjadala juu ya kukosekana kwa teknolojia ya mstari wa goli kwenye mikikimikiki ya La Liga.

Kikosi cha Barca chini ya Xavi kilifunga bao la pili kupitia kwa mtokea benchi Fermin Lopez, aliyetumia pia makosa ya kipa Lunin kufunga.

Lakini, Barca ilishindwa kulinda uongozi wa goli, Vazquez alifunga kuisawazishia Los Blancos akimaliza krosi matata ya Vinicius. Na baada ya hapo, zikafuata nyakati matata za Bellingham; kijana wa kutoka Birmingham, aliyefunga kwa mguu wa kushoto baada ya krosi ya Vazquez na hapo Real Madrid ikawa mbele 3-2 Santiago Bernabeu.

Ushindi huo umeifanya Real Madrid sasa kuweka pengo la pointi 11 kileleni kwenye msimamo wa La Liga dhidi ya Barcelona huku kila timu ikiwa imebakiza mechi sita kutimisha msimu huu. Hiyo ina maana, ushindi kwenye mechi tatu tu zijazo utatosha kuwafanya Los Blancos kuwa mabingwa wa La Liga kwa msimu huu wa 2023-24.

Kutokana na hilo, hii hapa orodha ya waliotamba na kuchemsha kwenye kipute hicho cha Santiago Bernabeu...

AMETAMBA: Jude Bellingham
Bellingham bila shaka atakuwa anazifurahia mechi za Barcelona. Hilo ni kutokana na namba nzuri anazopata kwenye El Clasico, kwamba ni kama ni mechi anazoziwezea vyema kabisa. Mara zote tatu alizokabiliana na Barcelona msimu huu, Bellingham amefanya jambo na kuiweka timu yake kwenye nyakati nzuri.
Oktoba mwaka jana, Bellingham aliishika mwenyewe mechi ya El Clasico, ambapo alifunga mara mbili kipindi cha pili, ikiwamo kwenye dakika za majeruhi, Los Blancos iliposhinda 2-1 kwenye Uwanja wa Olympic. Alionyesha makali pia kwenye fainali ya Spanish Super Cup, ambapo aliasisti bao la Vinicius - wakati Real Madrid ilipowachapa wapinzani wao hao huko Saudi Arabia.
Na Jumapili, alifunga bao la ushindi na hivyo kuisogeza timu yake kwenye hatua nzuri ya kunyakua ubingwa wa La Liga msimu huu, huku akifunga mabao 21 kwenye La Liga na 30 kwenye michuano yote.

AMECHEMSHA: Frenkie de Jong
Bahati mbaya kiasi gani kwa De Jong. Kiungo huyo wa Kidachi alionekana kutuliza daluga zake na kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Barca tangu msimu uliopita, lakini msimu huu amekuwa akisumbuliwa sana na majeraha. Kwa kuanzia Agosti mwaka jana, wakati alipopata maumivu ya enka, Jumapili alipata majeraha mengine ya mguu na matokeo yake alitolewa uwanjani. Bahati mbaya kwa De Jong. Kikosi cha Xavi kina shida nyingi, lakini kumkosa kiungo huyo sehemu ya katikati ya uwanja ni pigo kubwa kubwa. Bila ya huduma yake, Barca haipo vizuri. Lakini, hilo ni pigo pia kwake binafsi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea michuano ya Euro 2024.

AMETAMBA: Lucas Vazquez
Si shujaa aliyetarajiwa kwenye El Clasico, lakini Vazquez alikuwa mtu ambaye Real Madrid ilimhitaji kwenye mchezo huo ili kupata mafanikio. Kwenye ulinzi, staa huyo wa kimataifa wa Hispania alimdhibiti kwelikwlei Raphinha, hakumpa kabisa nafasi Mbrazili huyo kufurukuta. Aling'ara upande wa kulia kuisawazishia Madrid, ambapo alimvuka Joao Cancelo na kumzidi ujanja Cubarsi kupata penalti iliyofungwa na Vinicius. Baadaye, alifunga bao la pili la Los Blancos na kisha alitengeneza bao la ushindi. Licha ya kwamba sifa nyingi zinakwenda kwa Bellingham, lakini Varquez alionyesha ubora mkubwa kweye mchezo huo matata kabisa.

AMECHEMSHA: La Liga
Kwenye mchezo wa El Clasico, La Liga imeumbuka kwa kukosekana kwa teknolojia ya goli, ambayo ilizua utata baada ya Barcelona kufunga bao na kisha VAR kulikataa kwa madai kwamba mpira haujavuka mstari. Ukweli ni kwamba bado hakuna uhakika kama mpira ulivuka mstari kuwa bao au haukuvuka, hivyo La Liga inapaswa kuwekeza kwenye kuweka teknolojia ya kwenye magoli. Rais wa La Liga, Javier Tebas alitetea kwamba matukio ya aina hiyo huwa hayatokei mara kwa mara hivyo, hicho ndicho kitu ambacho kiliwafanya wasiharakishe kuweka teknolojia huyo ya goli. Lakini, kwa kilichotokea Jumapili na kwa kuwa kimeikuta timu kubwa basi huenda mabadiliko yatafanyika.

AMETAMBA: Carlo Ancelotti
Mara zote ushindi wa El Clasico ni mzuri, lakini huu wa Jumapili ulikuwa mzuri zaidi kwa kocha Ancelotti kwa sababu unamsogeza kwenye ubingwa wa La Liga msimu huu. Madrid ina kitu kingine cha kukitazama kwenye msimu huu, si tu kushinda taji la 15 la Ligi ya Mabingwa Ulaya, bali kushinda mechi zilizobaki kwenye ligi ili kunyakua ubingwa na kumpa nafasi kocha Ancelotti kufikiria mambo yajayo.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid itakipiga na Bayern Munich katika hatua ya nusu fainali, ambapo mchezo wa kwanza utapigwa Aprili 30 na mechi ya marudiano itapigwa siku nane baadaye. Hivyo, ushindi wa kwenye El Clasico, unampa wakati mzuri kocha Ancelotti katika kukiandaa kikosi chake katika kuwakabili Bayern Munich, ambao ni wapinzani wagumu kwenye mikikimikiki hiyo ya Ulaya.

AMECHEMSHA: Xavi
Ndani ya siku tano, kila kitu kimekwenda hovyo. Kikosi cha Barca chini ya kocha Xavi kilisukumwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Paris Saint-Germain na wakati wakiwa bado kwenye maumivu hayo, wamekujikuta akichapwa na Real Madrid na hivyo kuwekwa mbali kabisa na ndoto za kutetea ubingwa wao wa La Liga msimu huu.

Katika mchezo wa Jumapili, kocha Xavi alitarajia kupata huduma nzuri kutoka kwa wachezaji wake wa kubwa, ambao wangecheza El Clasico kikubwa, kama Robert Lewandowski, Ilkay Gundogan, Pedri na Raphinha na wengine, lakini mambo hayakuwa vizuri kabisa, kocha huyo Mhispaniola alishindwa kutafuta namna nzuri ya kupata matokeo mazuri kutoka kwa wachezaji hao ili kushinda mchezo.