Utamu wa UEFA umefikia hapa, Atalanta ikiishangaza Dormtund
Muktasari:
- Katika mechi za jana, imeshuhudiwa Atalanta ikipindua meza mbele ya Borussia Dortmund, kwani mechi ya kwanza ilifungwa 2-0, ikaja kushinda 4-1 na kufuzu kwa mabao 4-3.
JANA Jumatano zimechezwa mechi nne za mtoano katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kukamilisha idadi ya timu 16 ili kuanza mchakamchaka wa hatua inayofuata kwenye michuano hiyo. Hiyo ni baada ya juzi Jumanne pia kuchezwa mechi nne za mtoano.
Katika mechi za jana, imeshuhudiwa Atalanta ikipindua meza mbele ya Borussia Dortmund, kwani mechi ya kwanza ilifungwa 2-0, ikaja kushinda 4-1 na kufuzu kwa mabao 4-3.
Juventus licha ya kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Galatasaray, lakini imeshindwa kutoboa kutokana na awali ugenini kufungwa 5-2, hivyo imeondoshwa kwa jumla ya mabao 7-3.
Real Madrid imeichapa tena Benfica inayofundishwa na Jose Mourinho kwa mabao 2-1 baada ya kuipiga awali 1-0 ugenini, huku PSG na Monaco zikitoka sare ya 2-2, lakini imekuwa faida kwa PSG baada ya mechi ya kwanza kushinda 3-2, hivyo imepenya kwa mabao 5-4.
Sasa baada ya hatua ya mtoano kukamilika rasmi, timu 16 zilizobaki sasa zinaelekeza macho yao kwenye droo itakayopanga njia kuelekea fainali. Zaidi ya kujua nani amefuzu, macho yote yako kwenye droo itakayochezeshwa kesho Ijumaa kupanga ratiba ya mechi za hatua ya 16 bora na kuendelea.
MADRID NA ATLETICO MACHO ENGLAND
Real Madrid ilimaliza kazi dhidi ya Benfica na sasa inasubiri mpinzani wake katika droo itakayofanyika kesho Ijumaa. Mabingwa hao wa Hispania, wanaweza kukutana na Manchester City chini ya kocha Pep Guardiola au Sporting CP, changamoto mbili tofauti lakini zenye uzito mkubwa kwa namna yake.
Kwa upande mwingine, Atlético Madrid imehakikishiwa kukutana na timu kutoka Ligi Kuu England. Kikosi cha kocha Diego Simeone kitamenyana ama na Liverpool au Tottenham Hotspur, zilizomaliza wa tatu na wa nne katika hatua ya Ligi.
BODO, PSG KATIKA MTIHANI MGUMU
Timu iliyoshangaza wengi, Bodo/Glimt, baada ya kuiondoa Inter Milan, sasa itakutana na vigogo. Inaweza kupangwa dhidi ya Manchester City au Sporting, zote zikiwa miongoni mwa timu bora katika hatua ya Ligi.
Mabingwa watetezi, Paris Saint-Germain, bado hawajafahamu mpinzani wao rasmi lakini wanaingia kwenye droo wakiwa na uwezekano wa kukutana na wapinzani wakubwa.
NEWCASTLE, LEVERKUSEN ZINASUBIRI VIGOGO
Newcastle United, baada ya kutawala mechi yao ya playoff, itakutana ama na Barcelona au Chelsea. Zote ni klabu zenye historia kubwa Ulaya ambazo zitapandisha kiwango cha ushindani kwa kikosi cha Eddie Howe.
Wakati huohuo, Bayer Leverkusen imepangwa kukutana na ama Arsenal au Bayern Munich, zilizomaliza wa kwanza na wa pili katika hatua ya Ligi. Mpinzani yeyote kati yao atakuwa mtihani mkubwa kwa upande wa Wajerumani hao.
DROO ITAKAVYOBADILI MAMBO
Droo ya hatua ya 16 bora, robo fainali na nusu fainali itafanyika kesho Ijumaa, Februari 27, 2025 saa 9:00 alasiri. Washindi wanane wa playoffs wataungana na timu nane bora kutoka hatua ya Ligi, ambazo zinaingia kama timu zilizopangwa tayari kusubiri wapinzani.
Kwa kuwa wapinzani wanaowezekana sasa wamefahamika, UEFA Champions League inaingia katika hatua yake ya uamuzi makubwa zaidi. Kuanzia hapa, droo moja tu inaweza kubadilisha kila kitu.