Ushauri wa Gerrard kwa Arteta, akimsifia Declan Rice
Muktasari:
- Saka na Eze waliingia kipindi cha pili na kubadili kasi ya mchezo, jambo ambalo limemfanya Gerrard kuamini kuwa kuanza kwao kutatoa matokeo tofauti katika dimba la Emirates wiki ijayo.
GWIJI wa Liverpool, Steven Gerrard, amemshauri kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, kuanza na Eberechi Eze na Bukayo Saka kwenye mechi ya mkondo wa pili wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumanne ijayo.
Ushauri huo unakuja baada ya Arsenal kulazimishwa sare ya 1-1 na Atletico Madrid katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa jana Jumatano jijini Madrid, Hispania, huku Arteta akiwaweka benchi nyota hao wawili.
Akizungumza kupitia TNT Sports, Gerrard amesisitiza kuwa Arsenal inahitaji makali zaidi katika safu ya ushambuliaji ili kuvunja ngome ya Diego Simeone kwenye mechi ya mkondo wa pili.
"Katika mechi ya mkondo wa pili, ni lazima Eze awe uwanjani. Nadhani anaipa Arsenal ule mwanga wa ziada na anaonekana kuwa hatari zaidi," amesema Gerrard.
Kuhusu Bukayo Saka, Gerrard ameongeza: "Saka lazima aanze. Unawatumia wachezaji wako wa mechi kubwa kwenye mechi muhimu kama hii ya mkondo wa pili."
Licha ya sare hiyo, Gerrard hakusita kummwagia sifa kiungo wa Arsenal, Declan Rice, akitaja kiwango alichoonyesha katika dimba la Metropolitano kuwa ni cha hali ya juu.
"Nilidhani alikuwa imara sana, hasa katika kipindi cha kwanza. Alitawala mchezo akiwa na mpira na hata asipokuwa nao. Alicheza jukumu tofauti kidogo, akishuka chini zaidi katikati ya walinzi wa kati ili kusaidia kuanzisha mashambulizi," amechambua Gerrard.
Katika mechi ya mkondo wa kwanza, mabao yote mawili yalipatikana kwa njia ya penalti kupitia kwa Viktor Gyökeres upande wa Arsenal na Julián Alvarez upande wa Atletico Madrid.
Saka na Eze waliingia kipindi cha pili na kubadili kasi ya mchezo, jambo ambalo limemfanya Gerrard kuamini kuwa kuanza kwao kutatoa matokeo tofauti katika dimba la Emirates wiki ijayo.