Usajili wa Januari... Mikel Arteta ataja mchezaji anayemtaka
Muktasari:
- Arsenal itakuwa Emirates kukipiga na Manchester United kwenye mchezo wa raundi ya tatu ya Kombe la FA jioni ya leo Jumapili, lakini bado ipo kwenye harakati za kutafuta wachezaji kuboresha kikosi kwa ajili ya kushindana na Liverpool kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: KOCHA Mikel Arteta amesema Arsenal itasajili mchezaji ambaye ataweza kuleta manufaa haraka baada ya kunaswa tu dirisha hili la Januari.
Arsenal itakuwa Emirates kukipiga na Manchester United kwenye mchezo wa raundi ya tatu ya Kombe la FA jioni ya leo Jumapili, lakini bado ipo kwenye harakati za kutafuta wachezaji kuboresha kikosi kwa ajili ya kushindana na Liverpool kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England.
Arteta amekiri kikosi chake cha sasa kina ukomo, kina mapengo mengi yanayohitaji kuzibwa. Na hafahamu namna ya kufanya kutokana na wachezaji wengi dirisha hili la katikati ya msimu kuuzwa kwa pesa nyingi.
“Tunataka mtu ambaye atakuja kuleta madhara makubwa kwenye timu na kuleta kile ambacho hakipo,” alisema.
“Huo ndio ugumu uliopo kwenye dirisha hili. Mara zote tumekuwa tukijadili, lakini namna gani tutafanya maboresho kwenye timu. Mambo yamegeuka kwa sababu tumekuwa na majeruhi wachezaji muhimu, lakini mtu tunayemtaka ni yule atakuja kuleta tofauti. Tuna mapengo mengi ya kuziba.”
Arteta pia amemzungumzia vizuri kocha wa Manchester United, Ruben Amorim wakati wakielekea kumenyana, akisema kwamba anatarajia kukutana na upinzani mkali kutoka kwa mabingwa hao watetezi wa Kombe la FA, huku wao wakitaka kuwa mabingwa wa msimu huu.
“Ona wanavyocheza dhidi ya timu kubwa, wanafanya vizuri na kupata matokeo wanayoyataka,” alisema Arteta akiizungumzia Man United.
“Namfahamu vizuri, nilimfuatilia tangu yupo Ureno na kuna sababu kubwa kwa nini amefika hapo na anastahili. Kila kocha anateuliwa kwa sababu tofauti. Wakati mwingine kuja kuibadili timu. Kombe la FA ni sehemu ya historia yetu, tumeshinda mara 14. Ni michuano inayotuhusu hasa.”