Undav apiga mbili akitokea benchi, Ujerumani yafuzu mtoano
Muktasari:
- Mabingwa hao wa dunia mara nne, walijikuta wakipata wakati mgumu baada ya kuruhusu bao la dakika ya 30 lililofungwa na nahodha wa Ivory Coast, Franck Kessie. Hata hivyo, kocha Julian Nagelsmann alifanya mabadiliko muhimu na Undav akalipa imani hiyo kwa kufunga mabao mawili kipindi cha pili akicheza kwa dakika 30 pekee.
Mshambuliaji aliyeingia akitokea benchi, Deniz Undav, ameibuka shujaa wa Ujerumani baada ya kufunga bao la ushindi katika dakika ya 90+4 na kuiongoza timu hiyo kufanya comeback ya kusisimua dhidi ya Ivory Coast, ushindi uliowahakikishia nafasi katika hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia 2026.
Mabingwa hao wa dunia mara nne, walijikuta wakipata wakati mgumu baada ya kuruhusu bao la dakika ya 30 lililofungwa na nahodha wa Ivory Coast, Franck Kessie. Hata hivyo, kocha Julian Nagelsmann alifanya mabadiliko muhimu na Undav akalipa imani hiyo kwa kufunga mabao mawili kipindi cha pili akicheza kwa dakika 30 pekee.
Mshambuliaji huyo wa Stuttgart, alisawazisha katika dakika ya 68 akimalizia kwa ustadi krosi ya mchezaji mwenzake aliyeingia akitokea benchi, Nadiem Amiri. Kisha akafunga bao la ushindi dakika ya 90+4 na kuiacha Ivory Coast ikitoka uwanjani kichwa chini.
Undav aliendelea na kiwango chake bora baada ya pia kufunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao alipoingia akitokea benchi katika ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Curacao kwenye mchezo wao wa kwanza.
Licha ya kupoteza, Ivory Coast bado ina nafasi ya kufuzu mtoano kutoka Kundi E ikiwa itashinda dhidi ya Curacao katika mchezo wa mwisho wa makundi.
Kikosi cha Emerse Fae kilianza mchezo kwa nguvu na kasi kubwa mjini Toronto, lakini Ujerumani ndiyo iliyotengeneza nafasi nyingi zaidi za wazi za kufunga.
Ujerumani ilidhani imepata bao katika dakika ya 22 kupitia Aleksandar Pavlovic, lakini bao lake la kichwa lililofungwa baada ya mpira wa kona lilikataliwa kutokana na kosa dhidi ya kipa Yahia Fofana.
Baadaye Ivory Coast ilipata bao la kuongoza baada ya winga mwenye umri wa miaka 19, Yan Diomande, kumpasia Amad Diallo ambaye shuti lake la karibu lilizuiwa na Nathaniel Brown. Hata hivyo, Kessie aliuwahi mpira uliorudi na kuutumbukiza wavuni.
Wajerumani waliendelea kukumbana na mikasa baada ya bao la Kai Havertz kufutwa kutokana na Jamal Musiala kumfanyia faulo Emmanuel Agbadou katika mchakato wa bao hilo. Wakati huo huo, Christ Inao Oulai na Kessie walikosa nafasi nzuri zilizoweza kuiongezea Ivory Coast mabao.
Makosa hayo yaliigharimu Ivory Coast mwishoni mwa mchezo.
Kipa Yahia Fofana aliokoa mashuti ya Brown na Amiri katika dakika za mwisho, lakini hakuwa na cha kufanya dakika ya 90+4 wakati Undav alipoutuliza kwa ustadi mpira kutoka kwa Felix Nmecha kabla ya kuupiga na kumshinda kipa huyo, na kuipa Ujerumani ushindi katika sekunde za mwisho za mchezo uliopigwa Uwanja wa
Toronto mbele ya watazamaji 43,036.