Unai Emery aleta janjajanja yake EPL
Muktasari:
- Aston Villa ilianza msimu wa Ligi Kuu England kwa kumenyana na Newcastle United mchana wa jana Jumamosi, imekuwa haina makali sana kwenye dirisha hili la usajili kutokana na kubanwa na sera ya matumizi.
BIRMINGHAM, ENGLAND: KOCHA Unai Emery amesisitiza Aston Villa haitashindana kuwamo kwenye Top Seven msimu huu, lakini amesisitiza timu yake itajaribu kuzipa wakati mgumu timu zenye bajeti kubwa kwenye usajili.
Aston Villa ilianza msimu wa Ligi Kuu England kwa kumenyana na Newcastle United mchana wa jana Jumamosi, imekuwa haina makali sana kwenye dirisha hili la usajili kutokana na kubanwa na sera ya matumizi.
Staa wao Jacob Ramsey yupo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wake wa Pauni 39 milioni kwenda Newcastle, wakati Leon Bailey alitarajia kukosa mechi hiyo ya Jumamosi kwa kuwa naye anakaribia kuondoka.
Na wakati Aston Villa ikiwa haipo kwenye presha yoyote ya kuuza zaidi, kuna uwezekano wa kupata pesa kiasi fulani kabla ya dirisha halijafungwa Septemba 1.
Emery amekuwa na malengo makubwa msimu huu ikiwamo kuwamo kwenye michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
“Sisi sio washindani wa nafasi za juu, lakini bado tuna uwezo wa kutenga timu imana licha ya kwamba hatuna bajeti ya kutosha,” alisema Emery.
“Yatupasa kuwa washindani na wachezaji wetu na kuendelea kupambana, lakini hatuwezi kuwa washindani wa nafasi saba za juu.”
Aston Villa imekuwa kwenye zuio la kutumia pesa kwenye dirisha la usajili huu baada ya kuonekana kuvuka viwango vya Uefa juu ya udhibiti wa matumizi endelevu.
Uefa mwezi uliopita iliipiga Aston Villa faini ya Pauni 9.5 milioni kutokana na kukiuka sera hiyo ya mapato na matumizi na huenda adhabu ikawa kubwa zaidi kama jambo hilo halitakuwa limerekebishwa katika kipindi cha misimu mitatu ijayo.