UKIZUBAA UMEACHWA Ni vita ya kusaka tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa

Muktasari:
- Vita ya ubingwa imeshamalizika baada ya Liverpool kubeba taji. Vita ya kuchuana kubaki kwenye ligi, imekwisha kutokana na timu tatu zinazoshuka daraja tayari kufahamika. Vita pekee iliyobaki kwa sasa ni ile ya kuwania tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, ambapo tiketi yake inatoka kwa timu inayomaliza kwenye Top Five katika ligi.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya mechi za wikiendi iliyopita kwenye Ligi Kuu England na zile zilizofanyika Ijumaa, vita ya kuwania kuwamo kwenye Top Five imezidi kuwa kali na kufanya huo kubaki kuwa uhondo pekee uliosalia kwenye ligi.
Vita ya ubingwa imeshamalizika baada ya Liverpool kubeba taji. Vita ya kuchuana kubaki kwenye ligi, imekwisha kutokana na timu tatu zinazoshuka daraja tayari kufahamika. Vita pekee iliyobaki kwa sasa ni ile ya kuwania tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, ambapo tiketi yake inatoka kwa timu inayomaliza kwenye Top Five katika ligi.
Kuna timu sita zinazochuana kuwania tiketi nne za kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, kuanzia kwa timu inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo hadi inayoshika nafasi ya saba. Timu gani itatoboa?
Kuna tofauti ya pointi sita tu kati ya timu inayoshika namba mbili na saba kwenye msimamo huo, jambo linalofanya ushindani kuwa mkali wa kupata timu nyingine zitakazoungana na mabingwa Liverpool kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Nafasi za Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa timu za England kupitia msimamo wa ligi ni tano, lakini moja tayari imeshanyakuliwa na Liverpool, hivyo zimebaki nafasi nne, ambazo zitashindaniwa na timu sita. Kwa ujumla, kutakuwa na timu sita kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kutokea England, ambapo moja itakuwa ni kati ya Manchester United na Tottenham Hotspur ambazo zitachuana kwenye fainali ya Europa League, ambapo timu hizo zote mbili hazimo kwenye Top Five.
Arsenal ingeshakamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao endapo kama ingeshinda dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield. Lakini, mechi hiyo ilimalizika kwa sare, hivyo Arsenal bado haijakamatia tiketi ya Ulaya.
Washindani wao wengine kwenye msako huo wa kuwania tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni Newcastle United, Chelsea, Aston Villa, Manchester City na Nottingham Forest. Nani atatoboa?
Arsenal - Namba 2, pointi 68
Arsenal ililazimika kupambana kwenye kipindi cha pili dhidi ya Liverpool ili kupata pointi muhimu iliyowaweka kwenye nafasi nzuri ya kuendelea kubaki katika nafasi ya pili. Lakini, kikosi hicho cha Mikel Arteta kinahitaji kupata ushindi walau kwenye mechi moja kati ya mbili zilizobaki ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Mechi zake zilizosalia, itacheza na Newcastle United, ambao pia wanatafuta nafasi kwenye Top Five na kisha itamalizia na Southampton ugenini. Mechi dhidi ya Newcastle itachezwa Jumapili hii uwanjani Emirates.
Newcastle United - Namba 3, pointi 66
Pointi tatu dhidi ya Chelsea hazikutosha kwa Newcastle United kuing’oa Arsenal kwenye nafasi ya pili, lakini ilikaribia kabisa pointi za wapinzani wao hao katika mchakamchaka wa kuwania tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Kitu kizuri ni kwamba mchezo ujao utazikutanisha Newcastle na Arsenal kwenye Uwanja wa Emirates, ambapo baada ya matokeo ya mechi hiyo, msimamo wa ligi unaweza kuwa tofauti kabisa. Ushindi kwa Newcastle utawapandisha hadi katika nafasi ya pili na kuishusha Arsenal, ambayo itakuwa na mtihani wa kusaka ushindi kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Southampton katika mechi ya mwisho. Uzuri wa Newcastle mchezo wao wa mwisho utakuwa nyumbani dhidi ya Everton.
Chelsea - Namba 4, pointi 66
Kipigo cha Chelsea kwenye mechi ya Newcastle United kiliwauma kiasi cha kutosha, hivyo ilihitaji kushinda dhidi ya Manchester United ili kuweka hai matumaini ya kubaki ndani ya Top Five kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Kocha Enzo Maresca, sasa atakuwa na kazi moja tu ya kuhakikisha anashinda mechi moja iliyobaki kwenye ligi, ambayo ni mbaya kwa upande wao kwa sababu itakwenda kumenyana na mpinzani mwingine kwenye mbio hizo za kusaka tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Nottingham Forest, tena ugenini. Mechi za aina hiyo ndizo zinazofanya vita ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kuwa na kali kwenye Ligi Kuu England.
Aston Villa - Namba 5, pointi 66
Kipigo cha 4-1 kutoka kwa Crystal Palace, Februari mwaka huu kiliiacha Aston Villa kwenye nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu England, lakini sasa ipo kwenye mchakamchaka wa kufukuzia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Kwenye mechi tisa za mwisho, Aston Villa imeshinda nane na kupenya kwenye Top Five na hivyo kusubiri mchezo wao wa mwisho wa ligi kuamua hatima yao ya msimu huu. Baada ya kuwachapa Tottenham usiku wa Ijumaa, itamaliza msimu kwa kuikabili Manchester United ugenini. Kwa Aston Villa mechi hiyo ya Man United inawezekana kushinda, jambo linaloweza kuwafanya wafikishe pointi 69.
Man City - Namba 6, pointi 65
Manchester City kushindwa kupata ushindi dhidi ya Southampton kilikuwa kitu kilichoshangaza wengi, lakini kurudi kwa straika Erling Haaland kwenye kikosi kinaweza kuleta mabadiliko makubwa na kusaidia hali ya mambo. Kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola bado kila kitu kipo kwenye mikono yao juu ya kufahamu hatima ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Mechi yao ijayo itakipiga na Bournemouth uwanjani Etihad na kisha itamaliza msimu kwa kukipiga na Fulham ugenini. Ushindi kwenye mechi hizo, utaifanya Man City kufikisha pointi 71, ambazo zitatosha kuwapa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Nottingham Forest - Namba 7, pointi 62
Mtihani wa kwanza wa Nottingham Forest kwenye msako wa kuwania tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, utaanza kwa kipute cha ugenini kumenyana na West Ham United, Jumapili hii. Matokeo ya mechi za hivi karibuni yaliibua wasiwasi kwa miamba hiyo baada ya kuambulia pointi moja tu katika mechi hizo tatu ilizocheza uwanjani City Ground dhidi ya Everton, Brentford na Leicester City. Vita imekuwa kali, lakini ushindi kwenye mechi mbili za mwisho unaweza kuiweka Forest kwenye nafasi nzuri ya kukamatia tiketi ya michuano ya Ulaya, kwa sababu ina uwezo wa kufikisha pointi 68, ambazo baada ya hapo itatazamwa matokeo ya timu nyingine.
Mchezo wao wa mwisho, Forest itakipiga na Chelsea, ambayo pia imo kwenye vita hii ya kumaliza ndani ya Top 5 za kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.