Ngoja Alonso aje tuone

Muktasari:
- Kocha huyo Mhispaniola bila ya shaka atakuwa na mpango mkubwa wa nani atamhitaji kwenye kikosi chake cha Bernabeu na anaonekana kama atawasaidia kuwarudisha kwenye makali yao.
MADRID, HISPANIA: NI suala la muda tu kabla ya Xabi Alonso hajathibitishwa kuwa kocha mpya wa Real Madrid baada ya mwenyewe kutangaza kuachana na Bayer Leverkusen mwishoni mwa msimu.
Kocha huyo Mhispaniola bila ya shaka atakuwa na mpango mkubwa wa nani atamhitaji kwenye kikosi chake cha Bernabeu na anaonekana kama atawasaidia kuwarudisha kwenye makali yao.
Alonso ni moja ya makocha bora vijana na atakwenda Bernabeu kurithi kikosi chenye mastaa matata kabisa kama Kylian Mbappe, Jude Bellingham na Vinicius Jr, lakini anafahamu wazi kuna maeneo ya kuyafanyia maboresho pia. Kocha wa sasa wa Madrid, Carlo Ancelotti atakwenda kujiunga na timu ya taifa ya Brazil na hapo ataacha milango wazi ya Alonso kutua Bernabeu.
Swali muhimu linaloulizwa kwa sasa ni jinsi gani Real Madrid itatengeneza kikosi chake chini ya Alonso.
-Eneo la ulinzi; Kipa Thibaut Courtois bila shaka ataendelea kubaki golini na hilo halitabadilika chini ya Alonso, lakini itamlazimu kukuna kichwa juu ya mabeki wake, baada ya mabeki wa kati Antonio Rudiger na David Alaba wote wana umri wa miaka 32, licha ya kwamba bado wana kitu cha kufanya. Eder Militao naye ana matumaini makubwa ya kupata nafasi ya kucheza chini ya Alonso. Lakini, kunaweza kufanyika pia usajili wa beki wa kati, ambako kocha Alonso anapiga hesabu za kumnasa Jonathan Tah kutoka kwenye klabu ya Leverkusen, ambayo ataachana nayo mwishoni mwa msimu.
-Eneo la kiungo; Wakati Trent Alexander-Arnold anajihesabu kama beki, lakini anatazamiwa kwenda kucheza kwenye eneo la kati ya mabeki na viungo kwenye mtindo wa safu ya mabeki watatu inayotarajiwa kutumiwa na Alonso - la atatumika kama wing-back akipewa majukumu ya kushambulia kutokea pembeni. Kwenye upande mwingine wa uwanja, Alonso atatumia wing-back wa kushoto kwa kuzingatia huduma ya Ferland Mendy. Lakini, Alonso anaweza kusajili pia, akimsaka Alex Grimaldo kutoka Leverkusen, huku eneo la kiungo likitarajiwa kupambwa na Federico Valverde. Kwa kuwa Luka Modric umri umekwenda, Alonso anafikiria kumsajili Martin Zubimendi, ambaye pia anasakwa na Arsenal.
-Eneo la ushambuliaji; Kutafuta namna ya kuwatumia wote kwa ubora mkubwa baina ya Vinicius Jr na Kylian Mbappe litakuwa tatizo la kwanza Alonso analopaswa kulitatua. Alonso akishafahamu namna ya kuwatumia wachezaji hao atawapanga pamoja na Bellingham, atakayecheza kwenye Namba 10.