Kipa Martinez ashtua wengi

Muktasari:
- Hiyo ilikuwa mechi ya mwisho ya Aston Villa kwenye uwanja wa nyumbani na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, shukrani kwa mabao ya Ezri Konsa na Boubacar Kamara.
BIRMINGHAM, ENGLAND: KIPA Emi Martinez amemwaga machozi na kisha kuonyesha ishara ya kuaga kwa kuwapungia mkono mashabiki wa Aston Villa baada ya ushindi dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika uwanjani Villa Park, Ijumaa.
Hiyo ilikuwa mechi ya mwisho ya Aston Villa kwenye uwanja wa nyumbani na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, shukrani kwa mabao ya Ezri Konsa na Boubacar Kamara.
Martinez, 32, alicheza mechi hiyo bila ya kuruhusu bao dhidi ya wana fainali hao wa Europa League. Lakini, mwisho wa mechi hiyo, kulikuwa na tukio la kipa huyo kusherehekea kiasi.
Kipa huyo Muargentina alionekana akifuta machozi na kuwapungia mkopo mashabiki kwa ishara ya kuwaaga. Kipa huyo wa zamani wa Arsenal amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia Saudi Arabia.
Mchambuzi wa Sky Sports, Jamie Redknapp alisema: "Ulikuwa usajili bora sana. Ni mchezaji wa aina yake, ni kipa mahiri, lakini ni kama alikuwa anaaga. Kumpata mtu wa kuziba pengo lake ni ngumu."
Mchambuzi mwingine na kiungo wa zamani wa Manchester United, Roy Keane alisema hilo litakuwa pigo kubwa, aliposema: "Alikuwa mtu mwenye mipango, sawa ni mtu aliyekuwa akiwaudhi wengi kwa mambo yake, lakini ukweli alikuwa kipa bora na kuondoka ni pigo kubwa."
Kocha wa Aston Villa, Unai Emery alipoulizwa kuhusu hatima ya kipa huyo kwa kile alichokifanya baada ya mechi, Mhispaniola huyo alishindwa kuhakikishia mashabiki kama Martinez atabaki kwenye timu. "Martinez amekuwa kipa bora Aston Villa tangu alipotua akitoka Arsenal kwa Pauni 20 milioni mwaka 2020 na alishinda tuzo ya kipa bora wa mwaka Yashin Trophy mwaka 2023 na 2024.