Ujerumani yamtibulia Otto Addo, atimua Black Stars
Muktasari:
- GFA imemuachisha kazi Otto, jambo linalowaacha wachezaji wakisikilizia nani atachukua mikoba yake kwa ajili ya maandalizi ya fainali hizo zinazopigwa Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 11 hadi Julai 19, mwaka huu.
ACCRA, GHANA: SHIRIKISHO la Soka la Ghana (GFA), limemuachisha kazi kocha mkuu, Otto Addo, ikiwa ni miezi mitatu tu kabla ya fainali za Kombe la Dunia 2026, likiiacha Black Stars katika hali ya sintofahamu, muda mfupi baada kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Ujerumani katika mechi ya kirafiki.
GFA imemuachisha kazi Otto, jambo linalowaacha wachezaji wakisikilizia nani atachukua mikoba yake kwa ajili ya maandalizi ya fainali hizo zinazopigwa Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 11 hadi Julai 19, mwaka huu.
Uamuzi huo uliothibitishwa katika taarifa iliyotolewa jana, Jumanne, asubuhi ulikuja saa chache tu baada ya Ghana kupoteza 2-1 dhidi ya Ujerumani katika Uwanja wa MHP Arena mjini Stuttgart kikiwa ni kipigo cha nne mfululizo.
“Uamuzi huu unaanza kutekelezwa mara moja,” GFA ilisema, ikiongeza kuwa, “mwelekeo mpya wa kiufundi” kwa timu ya taifa utatangazwa kwa wakati unaofaa. Ghana sasa inakabiliwa na hali ya kutokuwa na kocha mkuu chini ya siku 75 kabla ya Kombe la Dunia.
Muda wa kuachishwa kazi kwa Otto unaakisi shinikizo lililoongezeka kufuatia matokeo mabaya mfululizo ikitanguliwa na kipigo cha aibu cha mabao 5-1 dhidi ya Austria huko Vienna, Ijumaa iliyopita.
Zama ya pili ya Addo katika uongozi imekuwa ikihusiana na tofauti kubwa ya matokeo katika kikosi hicho na kwa upande mmoja alileta ustahimilivu wa kufuzu Kombe la Dunia 2026 kwa ushindi mara sita na sare moja na kurejesha imani baada ya kipindi chenye changamoto kwa timu hiyo kutofuzu mashindano ya kimataifa.