Ujerumani yaiangushia mvua ya mabao Curacao
Muktasari:
- Mabingwa hao mara nne wa dunia walitangulia mapema dakika ya sita kupitia bao la Felix Nmecha, mchezaji aliyewahi kuchezea timu za vijana za England, aliyefunga kwa shuti kali.
HOUSTON, MAREKANI: UJERUMANI imeanza vyema kampeni yake ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuifunga Curacao mabao 7-1 katika mchezo wa Kundi E uliochezwa jijini Houston.
Mabingwa hao mara nne wa dunia walitangulia mapema dakika ya sita kupitia bao la Felix Nmecha, mchezaji aliyewahi kuchezea timu za vijana za England, aliyefunga kwa shuti kali.
Hata hivyo, Curacao, ambayo inashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia yake, iliwashangaza Wajerumani kwa kusawazisha dakika ya 21. Kiungo wa FC Zurich, Livano Comenencia, aliandika historia kwa taifa hili baada ya kupiga shuti la mguu wa kushoto kutoka nje ya eneo la penalti lililomgonga mchezaji na kumpita kipa mkongwe Manuel Neuer.
Curacao, taifa lenye wakazi takribani 155,000 pekee, lilionyesha ujasiri mkubwa dhidi ya moja ya timu kubwa zaidi duniani. Mshambuliaji Jurgen Locadia pia alidai penalti baada ya kuangushwa na Jonathan Tah, lakini mwamuzi alikataa maombi hayo.
Baada ya mapumziko ya kunywa maji katikati ya kipindi cha kwanza, Ujerumani ilijipanga upya na kurejesha udhibiti wa mchezo. Nico Schlotterbeck aliifungia Ujerumani bao la pili kwa kichwa kizuri kilichotokana na kona ya Nathaniel Brown.
Dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza, Kai Havertz aliongeza bao la tatu kwa mkwaju wa penalti baada ya Felix Nmecha kuchezewa madhambi ndani ya eneo la hatari na Riechedly Bazoer.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Jamal Musiala alifunga bao la nne sekunde 69 tu baada ya kuanza tena kwa mchezo, akimalizia pasi nzuri kutoka kwa Joshua Kimmich.
Nathaniel Brown naye aliandika jina lake kwenye orodha ya wafungaji kwa bao la tano baada ya kupokea mpira ulioguswa kwa ustadi na Deniz Undav.
Undav hakubaki nyuma kwani alifunga bao la sita kwa kumalizia pasi nyingine kutoka kwa Kimmich kabla ya kutoa pasi ya mwisho kwa Havertz aliyefunga bao lake la pili na la saba kwa Ujerumani dakika mbili kabla ya mwisho wa mchezo kwa mkwaju wa ustadi uliompita kipa Eloy Room.
Ushindi huo mkubwa unaifanya Ujerumani kuanza kwa nguvu katika Kundi E huku Curacao ikipewa somo katika mechi yake ya kwanza kabisa ya Kombe la Dunia.