Uholanzi, Hispania zafanya kweli tena Ulaya

Mchezaji wa Ghana Derek Boateng akiwa amembeba Asomoah Gyan baada ya Gyan kufunga bao la kusawazisha dhidi ya Uingereza katika mechi ya kitaifa ya kirafiki iliyofanyika kwenye uwanja wa Wembley mjini London
LONDON, England UHOLANZI imejiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu fainali za Euro baada ya kuizabua Hungary 5-3 wakati Hispania iliendeleza ushindi wa Kundi I kwa kuichapa Lithuania mabao 3-1. Hungary ilifunga mabao mawili ya harakaharaka na kuifanya timu hiyo kuwa mbele kwa mabao 2-1. Alikuwa Wesley Sniejder aliyefunga mawili kabla ya mkongwe, Ruud van Nistelrooy kufunga lingine, lakini mchezaji wa Hungary, Zoltan Gera alifanya matokeo kuwa 3-3 ndani ya dakika 15 katika mechi hiyo ya Kundi E. Dirk Kuyt alifunga mabao mengine mawili zikiwa zimesalia dakika 12 na kuifanya Uholanzi kufikisha pointi 18 kutokana na mechi sita, ikiwa ni pointi tisa zaidi ya Hungary na kujiweka katika nafasi nzuri ya kucheza fainali hizo mwakani. Sweden iko nafasi sawa na Hungary baada ya kuipiga Moldova 2-1. Hispania ilishinda mechi yake ya tano mfululizo huku kiungo wake, Xavi Hernandez, akifunga bao la utangulizi. Lithuania ilisawazisha dakika ya 57 kwa jitihata zilizosababisha Juanma Mata kujifunga. Mechi za juzi, 10 kati ya hizo ni kuwani kufuzu Euro 2012, wakati mechi zilizosalia zilikuwa za kirafiki. Australia ilifunga mabao mawili ndani ya dakika nne na kuilaza Ujerumani mabao 2-1, huku England ikiruhusu bao dakika za lala salama na kulazimishwa sare ya 1-1 na Ghana kwenye Uwanja wa Wembley katika mechi ya kimataifa ya kirafiki. Uruguay iliyoingia nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka jana, ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ireland, huku Italia ikiifunga 2-0 Ukraine na Ufaransa ikitoka suluhu na Croatia. Uhoplanzi, ambayo ilipata bao la kuongoza dakika ya 13 kupitia kwa Robin van Persie, iko katika mazingira ya kufuzu huku kocha, Bert van Marwijk akisema kuwa ngome imewaangusha kwa kasi fulani kuruhusu mabao. “Inatakiwa kuwa wastahimilivu na kucheza kwa nguvu,” alisema kocha wa Uholanzi, Bert van Marwijk. “ mchezo ulianza vizuri, tukafunga mabao lakini mambo yakabadilika. Tulipoteza mipira kirahisi.” Uholanzi iliyoitandika Hungary 4-0 wiki iliyopita, ilishindwa kujipanga na kupoteza mipira mingi hata kutoa nafasi kwa wapinzani wao kutawala. Hispania inayocheza pasi fupifupi za haraka, ilidai kushindwa kufanya kweli kwenye Uwanja wa Kaunas wakisema haukuwa na viwango. “Lakini haya ni matokeo muhimu, japokuwa uwanja ulikuwa mbaya,” Xavi alisema baada ya kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa 11 mfululizo kwa mechi zote. “Tumefikia malengo, na kuanzia hapa tunaweza kusonga mbele … timu imecheza vizuri.” Shuti la Xavi lilimgonga Andrius Skerla na kuingia wavuni na kuifanya Hispania kuongoza kwa bao la dakika ya 19 na walitengeneza nafasi nyingi kupitia kwa Fernando Llorente. Kipa Zydrunas Karcemarskas aliokoa mpira wa hatari wa Llorente mwanzoni mwa kipindi cha pili kabla ya Marius Stankevicius alipiga shuti katikati ya msitu wa wachezaji na kusawazisha bao. Hispania ikiwa na kiungo wake, Xavi alimchanganya beki wa Lithuania, Tomas Razanauskas na kumfanya ajifunge katika dakika ya 70. Kw amatokeo hayo, Hispania sasa ina pointi 15 ikiwa ni pointi sita zaidi ya Jamhuri ya Czech iliyoifunga Liechtenstein 2-0. Nayo Ubelgiji iliifunga Azerbaijan 4-1 na kushika nafasi ya pili katika Kundi A ikiwa ni pointi moja zaidi ya Uturuki, iliyoifunga Austria 2-0. Katika Kundi C, Serbia ilitoka sare ya 1-1 na Estonia huku Slovenia ikitoka suluhu na Ireland ya Kaskazini. Adrian Mutu alifunga mara mbili na kuiwezesha Romania kuifunga Luxembourg 3-1 katika mechi ya Kundi D, wakati Israel ilishinda 1-0 dhidi ya Georgia katika mechi za Kundi F. Mshambuliaji wa Bayern Munich, Mario Gomez aliipatia timu yake bao la kuongoza katika mechi hiyo iliyopigwa Moenchengladbach lakini David Carney akasawazisha dakika ya 61 na David Wilkshire akaifungia penalti ya bao la ushindi Socceroos. Australia ilipoteza mechi tatu mfululizo, na kuruhusu mabao matatu katika kila mechi. “Hatukutarajia matokeo haya,” alisema Holger Osieck, Kocha wa Australia. “Nawaheshimu Ujerumani, sikuangalia nani yuko uwanjani, wana wachezaji wazuri. Tulipanga kucheza vizuri na kujihami, lakini hatukutarajia matokeo haya.” Nayo Ufaransa ilikatizwa ushindi wa sita mfululizo baada ya Karim Benzema kupoteza nafasi ya wazi huku Adil Rami akiigongesha posti dhidi ya Croatia mechi iliyopigwa Stade de France. Giuseppe Rossi na Alessandro Matri waliifungia Italia mabao mawili na kuifanya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 huku ikicheza dakika 16 wakiwa 10 baada ya Davide Astori aliyeingia kipindi cha pili kulambwa kadi nyekundu. Kiungo wa FC Porto, Ruben Micael alifunga mabao mawili na kuiwezesha Ureno kushinda 2-0 dhidi ya Finland mjini Aveiro, lakini Russia ililazimishwa sare ya 1-1 na Qatar. Katika mechi nyingine, Denmark ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Slovakia huku Ugiriki ikitoka suluhu na Poland.