Uganda yawahi mapema Morocco
Muktasari:
- Timu hiyo iliondoka Kampala tangu Desemba 7 na ilitarajiwa kucheza mechi mbili za kujipima ngyuvu kabla ya kuanza vita ya fainali hizo ikipangwa Kundi C sambamba na Tanzania, Nigeria na Tunisia.
WAPINZANI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 Uganda The Cranes wamewahi mapema Morocco karibu siku 11 kabla ya kuanza kwa fainali hizo Jumapili hii.
Timu hiyo iliondoka Kampala tangu Desemba 7 na ilitarajiwa kucheza mechi mbili za kujipima ngyuvu kabla ya kuanza vita ya fainali hizo ikipangwa Kundi C sambamba na Tanzania, Nigeria na Tunisia.
Katika mahojiano ya hivi karibuni, kocha mkuu wa Uganda, Paul Put alionyesha kujiamini kuwa Uganda ina uwezo wa kufika hatua ya mtoano licha ya ukubwa wa wapinzani watakaokutana nao.
Akizungumzia kukutana na Super Eagles wa Nigeria, Put aliiambia mtandao wa CAF; “Nigeria ni moja ya timu kubwa barani Afrika kwa muda mrefu. Wanatisha kila sehemu ya uwanja, wakiwa na wachezaji wenye vipaji vikubwa na uzoefu wa kucheza Ulaya.
“Tunisia ni timu iliyopangwa vizuri sana, yenye ufundi na mbinu za hali ya juu. Ni ngumu kuwavunja, lakini tutaona. Tanzania, majirani zetu, wana mchanganyiko mzuri wa nguvu na kufahamiana, mechi za majirani hazikosi ugumu.”
“Tunaheshimu timu zote, lakini hatutishwi wala hatuogopi. Tutapambana na kuonyesha kiwango kizuri.”
Akieleza malengo ya Uganda huko Morocco, alisema: “Kimsingi tunataka kusonga mbele. Lakini kwanza tunataka kiwango chetu kioneshe soka la kisasa: uwiano mzuri, kujituma katika kila awamu ya mchezo, na uthabiti. Tukipata heshima mbele ya vigogo wa soka Afrika na kufuzu hatua ya mtoano, tutakuwa tumefanya kazi nzuri.”
Uganda itaanza kampeni yake dhidi ya Tunisia 'Carthage Eagles' kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah Desemba 23, kisha kuikaribisha Taifa Stars kwenye Uwanja wa Al Medina Desemba 27, kabla ya kumalizia mechi ya kundi dhidi ya Nigeria Desemba 30 katika Uwanja wa Fez.