Trent atoa masharti mawili kubaki Anfield
Muktasari:
- Mkataba wa sasa wa Alexander-Arnold utafika tamati mwishoni mwa msimu huu, hivyo kwa sasa yupo huru kusaini mkataba wa awali na klabu za ng'ambo.
LIVERPOOL, ENGLAND: BEKI wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold anahitaji mkataba mrefu pamoja na kukabidhiwa kitambaa cha unahodha ili abaki Anfield.
Mkataba wa sasa wa Alexander-Arnold utafika tamati mwishoni mwa msimu huu, hivyo kwa sasa yupo huru kusaini mkataba wa awali na klabu za ng'ambo.
Liverpool ilikataa ofa ya Pauni 20 milioni kutoka Real Madrid kwenye mkesha wa Mwaka Mpya 2025 kwa ajili ya mchezaji huyo.
Madrid inaonekana kuwa mstari wa mbele kwenye kufukuzia huduma ya mchezaji huyo ili wamchukue bure mwishoni mwa msimu. Lakini, kinachoonekana ni kama vile mchezaji huyo amewapa muda mabosi wa Liverpool kuamua kitu cha kufanya, lakini mwenyewe akihitaji mkataba wa muda mrefu.
Beki huyo wa kulia amejiunga na Liverpool tangu akiwa mdogo, akikulia kwenye akademia ya timu hiyo. Na sasa anaonekana bado anahitaji kubaki Liverpool kama timu hiyo itafuata masharti yake mawili.
Kwa mujibu wa talkSPORT, Alexander-Arnold anataka mkataba unaoanzia miaka mitatu ili kubaki kwenye timu hiyo, pia ihakikishe inamfanya kuwa nahodha wa kikosi hicho. Nahodha wa sasa wa kikosi hicho, Virgil van Dijk naye mkataba wake unafika tamati mwishoni mwa msimu.
Na sasa haifahamiki kama sharti la pili la Alexander-Arnold litaathiri mazungumzo ya dili jipya linalomhusu Mdachi huyo huko Anfield.
Van Dijk ana umri wa miaka 33, hivyo Alexander-Arnold anaamini ndoto zake za kuwa nahodha kwenye kikosi hicho zitatimia kwa sababu beki huyo Mdachi hata kama ataongeza mkataba mpya, basi hauwezi kuwa mrefu sana. Lakini, endapo kama atatimkia zake Real Madrid, basi huko anakwenda kulipwa mshahara wa Pauni 400,000 kwa wiki.