Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TORI PENSO: Mama watoto watatu aliyeweka rekodi Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Achana na matokeo ya Afrika Kusini iliyotoka sare ya bao 1-1 na Czechia, rekodi nyingine imeandikwa na mwamuzi wa Marekani, Tori Penso ambaye ameingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa mwanamke wa pili katika historia kuchezesha mechi ya Kombe la Dunia la wanaume kama mwamuzi wa kati.

WAKATI Afrika Kusini ikijitetea katika mchezo wake wa pili wa Kombe la Dunia dhidi Jamhuri ya Czech kwenye Uwanja wa Mercedes-Benz jijini Atlanta, Marekani kuna rekodi ilikuwa ikiandikwa.

Achana na matokeo ya Afrika Kusini iliyotoka sare ya bao 1-1 na Czechia, rekodi nyingine imeandikwa na mwamuzi wa Marekani, Tori Penso ambaye ameingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa mwanamke wa pili katika historia kuchezesha mechi ya Kombe la Dunia la wanaume kama mwamuzi wa kati.

Kwa wengi, jina la Penso limeanza kusikika hivi karibuni lakini mafanikio hayo ni matokeo ya safari ndefu iliyoanza miongo kadhaa iliyopita katika jimbo la Florida nchini Marekani.

Jina lake kamili ni Mary Victoria Penso, ingawa duniani kote anafahamika zaidi kwa jina la Tori Penso. Alizaliwa Julai 8, 1986 katika mji wa Stuart uliopo Florida, eneo ambalo ndilo lilimjenga na kumkuza katika mazingira ya michezo.

Akiwa mtoto mdogo, Penso alipenda sana soka tofauti na wasichana wengi wa umri wake, muda mwingi aliutumia viwanjani akitazama mechi na kushiriki michezo ya vijana.

Mapenzi yake kwa soka yalimfanya aanze kucheza tangu akiwa na umri wa miaka 10 lakini maisha yalikuja kumbadilishia mwelekeo baada ya kugundua kipaji kingine tofauti na kucheza.

Akiwa na miaka 14, alianza kazi ya uamuzi wa mechi za vijana. Kile kilichoonekana kama kazi ya muda mfupi ya kujipatia fedha za matumizi binafsi baadaye kiligeuka kuwa taaluma iliyobadilisha maisha yake.

Katika mahojiano mbalimbali, Penso amewahi kueleza kuwa mama yake ndiye aliyemshawishi kujaribu kuwa mwamuzi, akiamini kuwa angeweza kujifunza nidhamu, kujiamini na kujitegemea mapema.

Kadri miaka ilivyopita, uwezo wake wa kusimamia mechi ulianza kuonekana wazi. Alikuwa na uthubutu wa kufanya maamuzi magumu na uwezo wa kudhibiti mechi bila kuogopa chochote.

Akiendelea na safari yake ya michezo, hakuchukulia poa elimu, alisoma Florida State University ambako alipata shahada katika masuala ya biashara na masoko ya kidijitali.

Baada ya kuhitimu, aliwahi kufanya kazi katika kampuni mbalimbali maarufu duniani zikiwemo Coca-Cola na Red Bull, jambo linaloonyesha kuwa mafanikio yake hayakuishia katika soka pekee.

Pia aliongeza maarifa kwa kupata Shahada ya Uzamili ya Biashara (MBA), hatua iliyompa uwezo wa kuunganisha taaluma na michezo kwa wakati mmoja.

Hata hivyo, moyo wake uliendelea kuvutwa na soka, aliendelea kupanda ngazi za uamuzi katika mashindano mbalimbali ya ndani Marekani hadi kufikia ligi kubwa zaidi za ushindani.

Mwaka 2013 alipata beji ya FIFA, hatua iliyomruhusu kuchezesha mechi za kimataifa na kuanza kujijengea jina nje ya Marekani.

Miaka saba baadaye aliandika historia kubwa alipokuwa mwanamke wa kwanza katika zaidi ya miaka 20 kuchezesha mechi ya Ligi Kuu Marekani maarufu kama Major League Soccer (MLS), moja ya ligi kubwa zaidi Amerika Kaskazini.

Hatua hiyo ilifungua milango mingine mingi, akaanza kupewa mechi za Ligi ya Mabingwa ya CONCACAF, michuano ya timu za taifa na mashindano mengine makubwa yanayosimamiwa na FIFA.

Mwaka 2021 aliweka rekodi nyingine kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuchezesha mechi ya kufuzu Kombe la Dunia ya wanaume katika ukanda wa CONCACAF, jambo lililoonyesha jinsi viongozi wa waamuzi walivyokuwa wakimuamini.

Umaarufu wake ulifikia kiwango cha juu zaidi mwaka 2023 alipoteuliwa kuchezesha fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake kati ya Hispania na England nchini Australia. Hiyo ilikuwa moja ya mechi kubwa zaidi kuwahi kusimamiwa na mwamuzi kutoka Marekani.

Fainali hiyo ilimpa sifa nyingi kutoka FIFA, wadau wa soka na wachambuzi waliomsifu kwa utulivu wake, uwezo wa kusoma mchezo na kufanya maamuzi sahihi katika mazingira yenye presha kubwa.

Ndani ya familia yake, Tori ameolewa na Chris Penso ambaye pia ni mwamuzi wa ngazi ya juu nchini Marekani. Wawili hao wamekuwa wakitajwa kama moja ya familia maarufu zaidi katika sekta ya uamuzi wa soka nchini humo.

Licha ya majukumu ya kazi na safari nyingi za kimataifa, Penso pia ni mama wa watoto watatu. Mara kadhaa amekiri kuwa jukumu la uzazi limemfundisha uvumilivu, mawasiliano na uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka.

Katika Kombe la Dunia 2026, FIFA ilimpa jukumu la kusimamia mchezo kati ya Czech dhidi ya Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Mercedes-Benz wenye uwezo wa kubeba mashabiki 71,000.

Kwa kuchezesha mchezo huo, Penso alijiunga na kundi dogo sana la wanawake waliowahi kufikia hatua hiyo katika historia ya Kombe la Dunia la wanaume, akifuata nyayo za Stephanie Frappart wa Ufaransa aliyefanya hivyo mwaka 2022.