Penalti ya Mokoena yaipatia Afrika Kusini pointi muhimu Kombe la Dunia
Muktasari:
- Czechia ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya sita kupitia kiungo Michal Sadilek kwa shuti kali akipokea asisti ya Alexandr Sojka.
Afrika Kusini 'Bafana Bafana' imepata pointi ya kwanza katika fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Czech.
Czechia ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya sita kupitia kiungo Michal Sadilek kwa shuti kali akipokea asisti ya Alexandr Sojka.
Bao hilo limetokana na makosa ya safu ya ulinzi ya Bafana Bafana ambayo mabeki wake wameshindwa kujipanga kuidhibiti Czechia ikatengeneza shambulizi la haraka kupitia mpira wa kurusha.
Licha ya Bafana Bafana kutengeneza mashambulizi mengi ya kufunga, lakini ikashindwa kupata utulivu wa kuyatumia vyema.
Dakika ya 83 Bafana Bafana imefanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia mkwaju wa penalti iliyopigwa na kiungo Teboho Mokoena baada ya beki wa Czech kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Pigo kubwa kwa Bafana Bafana itamkosa Mokoena kwenye mchezo wa tatu wa makundi dhidi ya Korea Kusini baada ya kupata kadi ya pili ya njano ambayo itamlazimisha kuikosa Korea Kusini.
Kiungo huyo alipata kadi ya kwanza kwenye mchezo wa ufunguzi dhidi ya Mexico.
Bafana Bafana imekosa ushindi kwenye mchezo huo licha ya kuutawala.
Sare hiyo bado itailazimu Bafana Bafana kusalia nafasi ya nne kwenye kundi lao A, ikilingana na Czech, timu zote zikiwa zimetoka kupoteza michezo ya kwanza.