Tonali katikati ya Arsenal, Man City, huku wababe Italia wakichomoza
Muktasari:
- Mchezaji huyo aliyeng'ara katika msimu uliopita wa mashindano huko England pia yupo katikati ya Tottenham Hotspur ambayo imeshaanza kujadiliana na wawakilishi wake, lakini ikisikilizia zaidi namna wababe wa ligi, Arsenal na Man City wanavyoendelea kusuguana juu yake.
KIUNGO wa Newcastle Unite na Italia, Sandro Tonali yupo katikati mazingira magumu kuamua iwapo akubali kutia saini kuichezea Arsenal au Manchester City msimu ujao.
Mchezaji huyo aliyeng'ara katika msimu uliopita wa mashindano huko England pia yupo katikati ya Tottenham Hotspur ambayo imeshaanza kujadiliana na wawakilishi wake, lakini ikisikilizia zaidi namna wababe wa ligi, Arsenal na Man City wanavyoendelea kusuguana juu yake.
Tonali ambaye pia anawaniwa na AC MIlan pamoja na Inter Milan za Italia, alikuwa wa moto msimu uliopita kwenye kikosi hicho wakati ambao namba zake zilianza kuzishawishi timu mbalimbali kuanza kumfuatilia mchezaji huyo ambaye mkataba wake Newcastle United unatarajiwa kumalizika ifikapo Juni 30, mwakani. Msimu uliomalizika Ulaya alicheza dakika 4,019 katika mashindano yote England huku thamani yake ikitajwa kuwa Pauni 100 milioni.
Ruben Dias
REAL Madrid inapambana kumvuta beki wa kati wa Manchester City, Mreno Ruben Dias mwenye miaka 29, kwa dau la takribani Pauni 80 milioni ili kwenda kusaidiana na Ibrahima Konate ambaye tayari keshamalizana na wababe hao wa Hispania. Dias amekuwa na msimu bora Man City, lakini kwa msimu wa pili amekuwa akihitaji changamoto mpya nje ya kikosi hicho. Mchezaji anamaliza mkataba Man City Juni 30, 2029.
Marcus Rashford
MANCHESTER United inadaiwa kuzitajia timu mbalimbali kwa msisitizo kwamba thamani ya mshambuliaji wa kimataifa wa England, Marcus Rashford ni Pauni 40 milioni na si vinginevyo. Hata hivyo, inaelezwa kwamba imeondoa uwezekano wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 kujiunga na Liverpool au Manchester City, lakini ikizipa kipaumbele zaidi timu za nje ya England au zilizo nje ya Top Six EPL.
Mateus Fernandes
MANCHESTER United inawawania wachezaji wa West Ham, Mateus Fernandes na Crysencio Summerville, lakini West Ham inataka jumla ya Pauni 140 milioni kwa ajili ya kiungo Mreno, Fernandes mwenye umri wa miaka 21 na winga wa kimataifa wa Uholanzi, Crysencio mwenye miaka 24. Hata hivyo, Mashetani Wekundu wanakabiliwa na wakati mgumu wa kuwanasa nyota hao wanaotakiwa pia na timu zingine.
Manu Kone
ARSENAL inadaiwa kukubaliana masharti binafsi na kiungo wa kimataifa wa Ufaransa, Manu Kone, lakini bado haijakubaliana ada na AS Roma ambayo inataka Pauni 43.2 milioni. Kone ni mmoja wa viungo bora katika Ligi Kuu Italia (Serie A) kwa sasa na kwa muda mrefu kiwango chake kimeendelea kuinufaisha Roma inayopambana kurudi katika ubora wake. Mchezaji huyo anamaliza mkataba na timu hiyo Juni 30, 2029.
Marco Palestra
BEKI wa kulia wa kimataifa wa Italia na Atalanta, Marco Palestra, mwenye umri wa miaka 21 anadaiwa kuzigonganisha Manchester City na Chelsea ambazo inadaiwa kwamba zimeshawasiliana na mawakala wake, lakini timu hizo bado hazijaanza mazungumzo rasmi na Atalanta. Palestra ambaye ni miongoni mwa mabeki vijana wanaokuja juu kwa kasi katika siku za karibuni, mkataba wake unatarajiwa kumaliza Juni 30, 2029.
Lois Openda
EVERTON wanaangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Ubelgiji, Lois Openda, mwenye umri wa miaka 26 kwa mkopo wenye kipengele cha kumnunua kutoka RB Leipzig. Openda ni miongoni mwa wachezaji wasiokuwa na nafasi katika kikosi cha kwanza cha Juventus anakocheza kwa mkopo na imekuwa ikielezwa kwamba anataka kuondoka. Leeds na Nottingham Forest pia zinamtaka. Mkataba wake RB Leipzig unaisha Juni 30, 2028.
Angel Gome
KIUNGO wa kimataifa wa England, Angel Gomes, yupo huru kuondoka Marseille baada ya klabu hiyo kumruhusu kusaka timu nyingine kwa ajili ya msimu ujao. Marseille inadaiwa kuwa tayari kupokea ofa, huku timu mpya zilizopanda Ligi Kuu England ambazo ni Coventry na Hull zikiwa miongoni mwa zinazomfuatilia mchezaji huyo mwenye miaka 25 aliyecheza msimu uliopita akiwa kwa mkopo Wolves.