Steven Gerrard: Declan Rice na Jude Bellingham ndio viungo bora kwa sasa
Muktasari:
- Mshindi huyo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2005, anaamini Rice ameimarika sana tangu ajiunge na Arsenal. Pia ameeleza kwake ingekuwa changamoto ya kuvutia kucheza dhidi ya Bellingham.
Gwiji wa Liverpool, Steven Gerrard, amewataja Declan Rice wa Arsenal na Jude Bellingham wa Real Madrid kama viungo wawili bora wa Kiingereza kwa sasa katika soka la dunia.
Mshindi huyo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2005, anaamini Rice ameimarika sana tangu ajiunge na Arsenal. Pia ameeleza kwake ingekuwa changamoto ya kuvutia kucheza dhidi ya Bellingham.
Akizungumza kwenye YouTube channel ya "Rio Ferdinand Presents", Gerrard amesema: "Nadhani Declan Rice ni kiungo mzuri sana. Napenda mengi kumuhusu, napenda tabia yake, napenda namna alivyopiga hatua nyingine akiwa Arsenal. Anaongeza vitu vipya kwenye mchezo wake, nadhani angekuwa mpinzani mgumu, mwenye nguvu kwa kutoa changamoto nzuri.
"Jude Bellingham, kama angekuwa Ligi Kuu ya England, ningependa sana kushindana naye moja kwa moja, hatua hiyo hiyo ingekuwa ya kuvutia sana. Kwa mtazamo wangu, hao ndio wawili bora kwa sasa, lakini ifahamike haya ni maoni yangu binafsi."
Declan Rice amekuwa katika kiwango bora sana akiwa na Arsenal msimu huu, na anachukuliwa kuwa miongoni mwa viungo kamili zaidi kwenye Ligi Kuu ya England.
Kwa upande mwingine, Jude Bellingham amekuwa na wakati mgumu wa kiufundi na kiafya hivi karibuni, jambo lililosababisha kutemwa nje ya kikosi cha England kinachojiandaa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Wales leo Alhamisi Oktoba 9, 2025, na wiki ijayo itacheza dhidi ya Latvia, mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026.