Steven Gerrard sasa ni babu
Muktasari:
- Hilo limetokea baada ya binti mkubwa kabisa wa staa huyo wa zamani wa England, mrembo Lilly-Ella, 21, kujifungua mtoto wa kike, aliyezaa na mpenzi wake Lee Byrne.
LIVERPOOL, ENGLAND: GWIJI wa Liverpool, Steven Gerrard amekuwa babu kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 45.
Hilo limetokea baada ya binti mkubwa kabisa wa staa huyo wa zamani wa England, mrembo Lilly-Ella, 21, kujifungua mtoto wa kike, aliyezaa na mpenzi wake Lee Byrne.
Mrembo Lilly aliposti taarifa hiyo ya kufurahisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, akionyesha picha ya mpenzi wake Byrne akiwa kwenye korido za hospitali na kitenga cha mtoto. Na aliweka maelezo kwenye picha hiyo: “@Leebyrne 2 sasa ni 3”, na kuweka emoji ya moyo wa rangi ya pinki.
Gerrard alirejea Uingereza baada ya kuachana na kazi yake huko Saudi Pro League alikokuwa akiinoa Al Ettifaq, alipofikia makubaliano ya kusitisha mkataba wake, Januari 29. Mrembo Lilly na mpenzi wake Lee, wanaripotiwa kuanzisha uhusiano mwaka 2022 na wawili hao walitangaza kuwa kuna mtoto anakuja, Januari mwaka huu.
Lee alihamia kwenye eneo lenye makazi ya kitajiri Freshfield huko Merseyside, ndiko alikopata nafasi ya kufahamiana na mrembo Lilly. Na tangu wakati huo, Byrne amekuwa karibu na familia hiyo kiasi cha kumwita mke wa Gerrard, mrembo Alex kwamba ni mama yake wa pili. Lilly alizaliwa Februari 2004.
Steven na mkewe mrembo Alex, 42, ni wazazi wa watoto wengine watatu, mabinti wawili Lexie, 19, na Lourdes, 13, na wa kiume Lio, saba.
Kwa sasa, Gerrard ni mchambuzi wa soka kwenye kituo cha televisheni cha TNT Sport na alikuwa akihusishwa na mpango wa kwenda kuinoa timu yake ya zamani ya Rangers.