Sterling awatishia kisu wezi kwake
Muktasari:
- Winga huyo Mwingereza mwenye umri wa miaka 30 alikuwa nyumbani na familia yake ndipo aliposikia milango inavunjwa na wezi kuingia ndani wakati huo akiwa anasubiri kutazama mechi ya Chelsea dhidi ya Wolves, Jumamosi iliyopita.
LONDON, ENGLAND: STAA, Raheem Sterling alikabiliana na wezi waliovamia nyumbani kwake kwa kuwashikia kisu katika tukio la kutisha lililotokea hivi karibuni akiwa na familia yake.
Winga huyo Mwingereza mwenye umri wa miaka 30 alikuwa nyumbani na familia yake ndipo aliposikia milango inavunjwa na wezi kuingia ndani wakati huo akiwa anasubiri kutazama mechi ya Chelsea dhidi ya Wolves, Jumamosi iliyopita.
Kinachoelezwa ni kwamba wezi hao watano walivunja na kuingia nyumbani kwa Sterling huko Berkshire. Kwa ujasiri mkubwa, Sterling kwanza alihakikisha mpenzi wake, mrembo Paige Milian pamoja na watoto wao, Thiago, 8, na Thai Cruz, 6, wanakuwa salama kabla ya kupanda ngazi ndani humo kwenda kukabiliana na wezi hao.
Sterling alifanikiwa kuwakabili wezi hao na kukimbia bila ya kuiba chochote.
"Alichukua kisu jikoni na kwenda kukabiliana na wezi hao," kilibainisha chanzo cha taarifa hiyo.
"Kilikuwa kitu cha kutisha kidogo, lakini kilisaidia. Kundi hilo la wezi lilikuwa limepandaa juu huku wakiwa wamevalia maski. Lakini, waliogopa na kukimbia baada ya kumwona Raheem."
Wezi hao walivamia nyumbani hapo kati ya saa 12:30 jioni hadi saa 1:00 usiku, saa moja kabla ya mechi ya Chelsea kuanza, ambayo ilikuwa inaanza saa 2 usiku, Jumamosi.
Polisi inaamini kwamba wezi hao walidhani Sterling hatakuwapo nyumbani kwa maana atakuwa ameenda Stamford Bridge kutazama mechi hiyo ya The Blues.
Hii ni mara ya tatu katika kipindi cha miaka saba Sterling amekuwa akivamiwa na wezi baada ya matukio yaliyopita kumtokea nyumbani kwake Surrey na Cheshire.
Msemaji wa Sterling alisema: "Tunathibitisha kwamba Raheem Sterling alivamiwa na wezi wikiendi iliyopita. Tunachoweza kueleza ni kwamba yeye na watoto wake walikuwa nyumbani hapo kwa wakati huo wa tukio. Hata hivyo, kila kitu kipo salama, yeye na familia yake."