Staa wa Mali Afcon 2025 aivutia Man United
Muktasari:
- Mashetani Wekundu wamebadilisha kwa kiasi kikubwa safu yao ya ushambuliaji ikilinganishwa na msimu uliopita. Katika Ligi Kuu England msimu uliopita, hakuna mchezaji wa Man United aliyefunga mabao zaidi ya 10, hali iliyochangia kumaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi.
CASABLANCA, MOROCCO: MANCHESTER United imeripotiwa kuwa katika mazungumzo mazito na mshambuliaji anayeshiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kuhusu uhamisho wa majira ya joto bila ya kulipa chochote.
Mashetani Wekundu wamebadilisha kwa kiasi kikubwa safu yao ya ushambuliaji ikilinganishwa na msimu uliopita. Katika Ligi Kuu England msimu uliopita, hakuna mchezaji wa Man United aliyefunga mabao zaidi ya 10, hali iliyochangia kumaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi.
Msimu huu, usajili wa Matheus Cunha, Bryan Mbeumo na Benjamin Šeško umeongeza uzalishaji wa mabao, na kwa sasa Man United ina safu ya ushambuliaji ya tatu bora katika ligi.
Hata hivyo, Mbeumo si sababu pekee inayowafanya Man United kufuatilia AFCON, kwani pia wanavutiwa na kiwango cha mshambuliaji wa Mali, Lassine Sinayoko.
Kwa mujibu wa AfricaFoot, Man United wameingia katika mazungumzo mazito na Sinayoko pamoja na mawakala wake.
Inaripotiwa kuwa mazungumzo yanaendelea vizuri, huku Man United wakitarajia kukamilisha dili la Sinayoko mwezi Januari, wakikamilisha makubaliano ya mshahara wa Euro 3 milioni kwa mwaka.
Man United inaweza kumsajili Sinayoko bila ada ya uhamisho itakapofanya hivyo katika dirisha la majira ya kiangazi, kwa kuwa mkataba wake wa sasa na klabu ya Ufaransa ya AJ Auxerre unamalizika mwisho wa msimu.
Iwapo Mashetani Wekundu watafikia makubaliano wakati wa dirisha la majira ya baridi, hilo litakuwa faida kubwa, hasa ikizingatiwa kuwa kipaji cha Sinayoko kimezivutia klabu kadhaa kubwa barani Ulaya.
Mshambuliaji huyo alianza AFCON 2025 vizuri, akifunga bao la kwanza la Mali katika sare ya 1-1 dhidi ya Zambia, kabla ya kufunga tena dhidi ya Morocco kwenye mechi iliyofuata.
Hayo yanafuatia kiwango kizuri cha klabu msimu huu, ambapo mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, ambaye mara nyingi amecheza kama mshambuliaji wa kati, amefunga mabao sita na kutoa asisti mbili huko Auxerre.
Katika mechi zake tatu za mwisho kabla ya kwenda AFCON, Sinayoko alifunga mabao matatu na kutoa asisti moja.
Itakuwa faida kwa United endapo Mmali huyo atajiunga, kwani ana uwezo wa kucheza maeneo yote ya mbele ya uwanja. Amecheza pande zote mbili za winga pamoja na nafasi ya mshambuliaji wa kati msimu huu.
Kwa matokeo hayo, endapo kiwango cha Cunha au Mbeumo kitashuka, Sinayoko atakuwa chaguo mbadala katika nafasi zao, lakini zaidi atakuwa mpinzani mkuu wa Benjamin Sesko katika nafasi ya mshambuliaji wa kati.