Staa Olympiacos, Ugiriki afariki dunia
Muktasari:
- Antzas amepoteza maisha baada ya kupambana na ugonjwa unaoathiri mfumo wa neva na misuli.
Soka la Ugiriki limeingia katika majonzi baada ya kifo cha beki wa zamani wa kati wa timu ya taifa ya nchi hiyo na klabu ya Olympiacos, Paraskevas Antzas, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 49.
Antzas amepoteza maisha baada ya kupambana na ugonjwa unaoathiri mfumo wa neva na misuli.
Hayati Antzas anakumbukwa kama nguzo kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati wa vipindi vyake viwili vya mafanikio ndani ya Olympiacos.
Katika kipindi chake cha uchezaji alitwaa mataji saba ya Ligi Kuu Ugiriki (Super League) na vikombe vitatu vya Kombe la Ugiriki akiwa na miamba hiyo ya jiji la Piraeus.
Kufuatia msiba huo, Olympiacos imetoa taarifa ikimuelezea Antzas kama mchezaji aliyetumia nguvu na hadhi yake kubwa kuheshimu jezi ya timu hiyo na imetuma salamu za rambirambi kwa familia na ndugu wa marehemu, ikimuombea apumzike kwa amani.
Kihistoria, Antzas alianzia soka katika timu ya vijana ya Pandramaikos kabla ya kung'ara zaidi akiwa na Xanthi. Uwezo wake ulimfanya asajiliwe na Olympiacos 1998, ambapo aliisaidia kutwaa mataji matano ya ligi mfululizo kabla ya kutangaza kustaafu 2003 kwa sababu za kifamilia.
Hata hivyo, alibadili uamuzi na kurejea uwanjani akiwa na klabu ya nyumbani kwao ya Doxa Drama na kisha Xanthi, hatua iliyomfanya akose michuano ya Euro 2004 ambayo Ugiriki ilitwaa ubingwa licha ya yeye kushiriki kikamilifu kwenye mechi za kufuzu.
Alirejea tena Olympiacos 2007 na kucheza hadi alipotundika daruga 2009, akihitimisha jumla ya mechi karibu 200 klabuni hapo. Pia aliwahi kuichezea timu ya taifa ya Ugiriki mara 26.