Staa Mexico aandika rekodi akifuata nyayo za Philipp Lahm
Muktasari:
- Nyota huyo anayeichezea Al-Qadsiah ya Saudi Arabia ameifungia Mexico bao la kwanza dakika ya tisa dhidi ya Afrika Kusini katika mechi ya kwanza ya ufunguzi.
MSHAMBULIAJI wa Mexico aliyezaluwa Colombia, Julian Andres Quinones, amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao katika fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazopigwa Marekani, Mexico na Canada.
Nyota huyo anayeichezea Al-Qadsiah ya Saudi Arabia ameifungia Mexico bao la kwanza dakika ya tisa dhidi ya Afrika Kusini katika mechi ya kwanza ya ufunguzi.
Bao hilo la nyota huyo ni la mapema zaidi kufungwa tangu Philipp Lahm alipoifungia Ujerumani katika fainali za Kombe la Dunia 2006.
Katika fainali za 2006, Lahm aliifungia Ujerumani bao dakika ya sita katika ushindi wa mabao 4-2, dhidi ya Costa Rica, likiwa ni la mapema zaidi katika historia ya mashindano hayo.
Pazia la fainali za Kombe la Dunia 2026 limefunguliwa leo kwa mechi baina ya wenyeji Mexico dhidi ya Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Azteca kuanzia saa 4:00 usiku.
Mechi hiyo ni mwanzo wa uhondo na msisimko wa tukio hilo kubwa la soka duniani ambalo litafikia tamati Julai 19, mwaka huu kwa mechi ya fainali itakayofanyika kwenye Uwanja wa MetLife, New York, Marekani.
Ni ufunguzi unaoleta ukumbusho wa fainali za Kombe la Dunia 2010 ambazo zilifanyika Afrika Kusini ambazo mechi ya kufungua mashindano ilizikutanisha timu hizi mbili za leo na ilimalizika kwa sare ya bao 1-1, Juni 11, 2010.