Son awasubirisha Wamarekani

Muktasari:
- Klabu hiyo ya ligi ya MLS ilikuwa inahitaji kwa nguvu zote huduma ya mkali huyo wa Korea Kusini ikitaka akambadili staa wa zamani wa Arsenal na Chelsea, Olivier Giroud, 38, ambaye amekwenda kujiunga na Lille ya Ufaransa.
LOS ANGELES, MAREKANI: KLABU ya soka ya Los Angeles FC ya Marekani italazimika kusubiri kwa muda kwenye mchakato wa kunasa saini ya nahodha wa Tottenham Hotspur, Son Heung-min.
Klabu hiyo ya ligi ya MLS ilikuwa inahitaji kwa nguvu zote huduma ya mkali huyo wa Korea Kusini ikitaka akambadili staa wa zamani wa Arsenal na Chelsea, Olivier Giroud, 38, ambaye amekwenda kujiunga na Lille ya Ufaransa.
Lakini, uhamisho wa kwenda Marekani hauonekani kuwapo kwa Son kwa sasa, jambo hilo linafanya miamba hiyo ya California kuwa na subira hadi Januari au kwa miezi 12 mingine ili kumchukua.
Son, ambaye atatimiza umri wa miaka 33 Jumanne, ameweka milango yake ya kuzifikisha mwisho nyakati zake kwenye klabu ya Spurs akitaka kuhama dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya kunyakua ubingwa wa Europa League.
Mkataba wake wa sasa unaomshuhudia akilipwa Pauni 200,000 kwa wiki umebakiza mwaka mmoja, lakini ishu ya kuhamia Marekani kwa sasa haipo kwenye mpango wake.
Fowadi huyo anatararajia kurudi mazoezini wiki ijayo kwa ajili ya kufanya vipimo vya afya. Na baada ya hapo Son atafanya mazungumzo na kocha mpya wa miamba hiyo, Thomas Frank.
Staa huyo wa kimataifa wa Korea Kusini amekuwa akiwindwa pia na klabu za Saudi Pro League, lakini siku za karibuni alikuwa akidaiwa kutakiwa na kocha wake wa zamani, Jose Mourinho huko kwenye klabu ya Fenerbahce ya Uturuki. Itakuwa uamuzi wa kushtua kama Spurs itaamua kumuuza kabla ya ziara yao ya kwenda Seoul, ambako ni kwao Son mapema Agosti.