Slot kupoteza watatu Liverpool
Muktasari:
- Majogoo hao kutoka Anfield wako katika njia nzuri ya kushinda taji la Ligi Kuu ya England katika msimu wa kwanza wa Arne Slot ikiwa na pointi sita zaidi ya Arsenal, walioko nafasi ya pili, lakini wao wana mchezo mmoja mkononi dhidi ya washika mitutu hao.
LIVERPOOL, ENGLAND: LICHA ya kuwa na msimu mzuri katika michuano yote ikiwa pamoja na kuongoza msimamo wa Ligi Kuu England, Liverpool inatarajiwa kuuza wachezaji watatu wa kikosi chao cha kwanza mbali ya wale wanaotarajiwa kuondoka baada ya mikataba yao kumalizika.
Majogoo hao kutoka Anfield wako katika njia nzuri ya kushinda taji la Ligi Kuu ya England katika msimu wa kwanza wa Arne Slot ikiwa na pointi sita zaidi ya Arsenal, walioko nafasi ya pili, lakini wao wana mchezo mmoja mkononi dhidi ya washika mitutu hao.
Katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, Liverpool ilifanya usajili mmoja tu wakimsajili winga Federico Chiesa kutoka Juventus kwa ada ya uhamisho ya Pauni 10 milioni.
Waliendelea kuwa na timu hiyo ambayo ilijengwa na Klopp kabla ya kuondoka, na hakukuwa na usajili mwingine katika dirisha la uhamisho la Januari lililofungwa hivi karibuni.
Licha ya kutokuwa na shughuli nyingi za usajili, ripoti mpya inaonyesha kuwa wachezaji watatu muhimu wanaweza kuondoka katika mabadiliko makubwa ya kikosi cha Slot kwa msimu ujao.
Kwa mujibu wa tovuti ya Anfield Watch, washambuliaji Diogo Jota, Darwin Nunez, na Luis Diaz wanaweza kuondoka katika miezi michache ijayo.
Ripoti hiyo inasema kwamba Nunez na Diaz wataweza kuwa kutimkia Ligi Kuu ya Saudi Arabia.
Diaz alijiunga na Liverpool akitokea FC Porto Januari 2022 kwa ada ya uhamisho ya Pauni 37.5 milioni, wakati Nunez akijiunga katika dirisha la majira ya kiangazi kwa ada ya Euro 85 milioni akitokea Benfica na
Jota alijiunga mwaka 2020 akitokea Wolves kwa Pauni 45 milioni.
Nunez ameifungia Liverpool mabao 39 katika michezo 127, wakati Diaz ameifungia mabao 36 katika michezo 130. Jota, kwa upande wake, ameifungia klabu mabao 64 katika michezo 165.
Mbali ya mastaa hawa, Liverpool pia huenda ikawakosa mastaa wake wengine watatu ambao ni Trent Alexander Arnold, Mohamed Salah na Virgil van Dijk ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa hawajasaini mikataba mipya.
Tofauti na ilivyokuwa kwa watatu wa kwanza ambao bado wana mikataba isiyopungua miaka miwili na wataondoka kwa kuuzwa, Salah, Van Dijk na Trent wanatarajiwa kuondoka bure.