Slot: Hii haijawahi kutokea hapa Liverpool
Muktasari:
- Mabingwa hao wa Ligi Kuu England sasa wamepoteza mechi nne mfululizo za ligi, wakiendelea kupoteza matumaini ya kutetea taji hilo waliloshinda msimu uliopita.
LIVERPOOL, ENGLAND: BAADA ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Brentford jana Jumamosi, Oktoba 25, Kocha wa Liverpool, Arne Slot amefunguka mechi hiyo ndiyo ilikuwa ya kwanza kwa wachezaji wake kucheza vibaya zaidi tangu achukue kazi ya kuifundisha timu hiyo.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu England sasa wamepoteza mechi nne mfululizo za ligi, wakiendelea kupoteza matumaini ya kutetea taji hilo waliloshinda msimu uliopita.
Katika mahojiano na waandishi wa habari, alipoulizwa kama hiyo ndiyo mechi mbaya zaidi tangu achukue mikoba ya kuifundisha Liverpool, Slot amesema: "Ndiyo, nafikiri ni mechi inayoongoza kwa wachezaji wangu kucheza vibaya tangu niwasili hapa.
*Kawaida huwa hata tukipoteza kwa bao moja au mawili, wachezaji huwa wanaonyesha hali ya kupambana, lakini mechi hii imekuwa tofauti, wakati pekee nilioona wachezaji wanapambana ni baada ya Brentford kutufunga bao la kwanza."
"Tulitarajia matokeo bora baada ya ushindi wa katikati ya wiki tuliopata katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Nilitarajia pia tutacheza vizuri zaidi, lakini kiwango tulichoonyesha ni kibovu sana, hata tulipokuwa tunapoteza mechi hapo awali, mara nyingi huwa tunacheza vizuri zaidi ya hivi leo."
"Hatukufanya mambo ya msingi inavyotakiwa. Tulipokuwa nyuma kwa bao 1-0, 2-0 au 3-1, nguvu ya mashabiki wao iliwasaidia. Ni timu nzuri katika kucheza mipira ya juu, lazima uwapongeza kwa hilo."
Hii ilikuwa ni wiki ya pili mfululizo kwa Liverpool kucheza na timu zinazotumia mbinu ya kucheza mipira mirefu na kuhusu hilo, Slot amesema bado anatafuta dawa yake.
"Wapinzani wana mtindo fulani wa kucheza dhidi yetu ambao kwa kweli unatusumbua na bado hatujapata suluhisho hadi sasa. Timu sasa zinajua namna ya kucheza dhidi yetu."