Slot apewa ujanja wa kumtema Salah
Muktasari:
- Fowadi huyo wa kimataifa wa Misri amekuwa na wakati mgumu kwenye kikosi hicho msimu huu akishangaza wengi baada ya msimu uliopita kucheza kwa kiwango cha juu sana.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA Arne Slot amepewa ujanja anaweza kutumia michuano ya Afcon kama nafasi muhimu kwake kufanya jaribio la kumtoa Mohamed Salah kwenye mipango yake katika kikosi cha Liverpool.
Fowadi huyo wa kimataifa wa Misri amekuwa na wakati mgumu kwenye kikosi hicho msimu huu akishangaza wengi baada ya msimu uliopita kucheza kwa kiwango cha juu sana.
Amefunga mabao matano katika mechi 16 za michuano yote, wakati msimu uliopita alifunga mara 34 wakati Liverpool iliponyakua ubingwa wa Ligi Kuu England.
Licha ya mafanikio hayo, kocha Slot alifanya maboresho makubwa kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo badaa ya kuwasajili Alexander Isak, Hugo Ekitike na Florian Wirtz kwa ada ya pamoja inayokaribia Pauni 250 milioni. Uhamisho huo umeshindwa kuleta mafanikio makubwa, huku Ekitike akionekana walau ndiye pekee ameonyesha kiwango katika hao fowadi wapya.
Salah anapambana kurudisha kiwango chake, jambo linalofanya kuwapo na kelele za kumtaka atupwe benchini. Na kiungo wa zamani wa Liverpool, Don Hutchinson anaamini Afcon, inayoanza mwezi ujao, utakuwa wakati mwafaka kwa Slot kuchezesha wachezaji wake wapya kwenye nafasi ya Mo Salah, ili hata staa huyo Misri atakaporudi, akute kuna ushindani wa nafasi.
Hutchinson amesema: “Kila timu kwenye Ligi Kuu England ingependa kuwa na Wirtz, Isak na Salah. Sasa ni kazi ya Slot kubadili mfumo na kujaribu kuwatumia wote hao kwenye kikosi cha kwanza, sambamba na Ekitike, kwa sababu huwezi kutumia pesa zote zile kwa Wirtz, Isak na Ekitike na kisha unawaambia wagombee namba.
"Mimi ningeshawishika kuwatumia wachezaji walio kwenye viwango bora kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu. Mjadala kwa nini unaendelea kuwa na Mo Salah kwenye timu. Michuano ya Afcon inakuja, nadhani ni muda wa kujaribu watu wengine!”
Kocha Arne Slot alizungumzia kiwango cha Mo Salah hasa zinapokuja nyakati za kuweka wasiwas wa kuhusu uwezo wake wa kufunga mabao, amesema: "Kitu kikubwa ni kwamba siku zote amekuwa akiifungia mabao Liverpool. Kitu cha mwisho kinachonipa shaka ni kuhusu Mo Salah kufunga mabao. Amekuwa akifanya hivyo maisha yake yote, bila shaka atafanya hivyo tena."