Shinda mechi zako! Ubingwa EPL Arsenal, Man City upo hapa
Muktasari:
- Arsenal inakabiliwa na mechi dhidi ya Newcastle United na Fulham, ambazo Merson amesema ni muhimu sana kushinda ili kuongeza presha kwa City.
LONDON, ENGLAND: MCHEZAJI wa zamani wa Arsenal, Paul Merson amesema mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England bado ziko wazi na Washika mitutu hao wana nafasi licha ya kushuka kileleni baada ya Manchester City kushinda dhidi ya Burnley.
Kwa sasa, Man City iko kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ikiwa nayo 66, huku Arsenal ikiwa nayo 63 na gwiji huo ambaye aliichezea pia timu ya taifa ya England amesema City walihitaji ushindi mkubwa dhidi ya Burnley ili kuonyesha ubabe wao, lakini walishindwa kutumia nafasi zao, jambo analosema limewapa Arsenal nafasi ya kurejea katika mbio hizo.
Ameongeza Arsenal ina mechi mbili kabla ya City kucheza tena na lazima wazitumie vizuri ili kujiweka mbele kwa presha.
Arsenal inakabiliwa na mechi dhidi ya Newcastle United na Fulham, ambazo Merson amesema ni muhimu sana kushinda ili kuongeza presha kwa City.
Kwa upande wa City, ina ratiba dhidi ya Everton, Brentford, AFC Bournemouth na Crystal Palace, pamoja na mchezo wa mwisho dhidi ya Aston Villa.
Merson amesema baadhi ya mechi hizo si rahisi kama zinavyoonekana, akitaja Everton na Brentford ni timu zinazopigania nafasi za Ulaya na Bournemouth kuwa na uimara wa kiulinzi.
Aliongeza ubingwa unaweza kuamuliwa na tofauti ya mabao, jambo linalofanya kila goli kuwa muhimu zaidi katika mechi zilizosalia.
“Arsenal bado wako kwenye mbio”
Merson amesema Arsenal ilipoteza mechi muhimu dhidi ya City, lakini bado hawajaondoka kwenye mbio za ubingwa.
Alieleza kikosi cha Arteta kilikosa bahati Etihad, ikiwemo Kai Havertz kukosa nafasi muhimu na shuti la Eberechi Eze kugonga mwamba wa lango.
Hata hivyo, alisisitiza makosa ya ulinzi ndiyo yaliyowagharimu zaidi, akimtaja Gabriel Martinelli kushindwa kumdhibiti mchezaji wa City wakati City inapata bao la ushindi lililofungwa na Erling Haaland.
Amesema katika kiwango cha ushindani wa juu kama huu, makosa madogo yanaweza kuamua ubingwa na wachezaji wanapaswa kuwa makini kila dakika.
Mbio za ubingwa bado wazi
Kwa mujibu wa Merson, City haijaonyesha ubora wa kuwatisha wapinzani wao kikamilifu na hivyo Arsenal bado wana nafasi ya kurudi kileleni iwapo watashinda mechi zao zijazo.
Amehitimisha kwa kusema kuwa mbio za ubingwa zinaweza kuamuliwa na mchezo mmoja au hata tofauti ya mabao, jambo linaloongeza msisimko mkubwa katika wiki za mwisho za msimu.
Mbio za Ubingwa EPL
Arsenal
(Mechi 33, pointi 70, tofauti ya mabao +37)
Jumamosi, Aprili 25 – Nyumbani dhidi ya Newcastle United
Jumamosi, Mei 2 – Nyumbani dhidi ya Fulham
Jumapili, Mei 10 – Ugenini dhidi ya West Ham United
Jumapili, Mei 17 – Nyumbani dhidi ya Burnley
Jumapili, Mei 24 – Ugenini dhidi ya Crystal Palace
Manchester City
(Mechi 33, pointi 70, tofauti ya mabao +37)
Jumatatu, Mei 4 – Ugenini dhidi ya Everton
Jumamosi, Mei 9 – Nyumbani dhidi ya Brentford
Jumapili, Mei 17 – Ugenini dhidi ya AFC Bournemouth
Ijumaa, Mei 22 – Nyumbani dhidi ya Crystal Palace
Jumapili, Mei 24 – Nyumbani dhidi ya Aston Villa