Shabiki United aliyegoma kunyoa afunguka
Muktasari:
- Frank Ilett, ambaye pia anasimamia ukurasa wa The United Strand, alihudhuria mechi ya Man United dhidi ya Chelsea wiki iliyopita ambayo ilimalizika kwa Mashetani Wekundu kushinda kwa mabao 2-1.
MANCHESTER, ENGLAND: SHABIKI wa Manchester United ambaye amekataa kukata nywele zake hadi timu hiyo ishinde mechi tano mfululizo amezungumza kuhusu shambulio alilopata kutoka kwa shabiki mwenzake.
Frank Ilett, ambaye pia anasimamia ukurasa wa The United Strand, alihudhuria mechi ya Man United dhidi ya Chelsea wiki iliyopita ambayo ilimalizika kwa Mashetani Wekundu kushinda kwa mabao 2-1.
Oktoba 5, mwaka huu Frank atakuwa anatimiza mwaka mmoja tangu aweke ahadi ya kutonyoa nywele hadi Man United ifikishe ushindi wa idadi hizo za mechi.
Hata hivyo, akiwa anazungumza na mashabiki wenzake kwenye eneo la mazungumzo, shabiki mmoja aliyeonekana kuwa na hasira alienda akamvuta nywele kwa nguvu huku akimtolea maneno machafu.
Mashabiki wengine walijaribu kuingilia kati, lakini wakati anaendelea kumvuta nywele alitumia mguu wake pia kumkanyaga. Akizungumza na tovuti ya The Sun baada ya tukio hilo, Frank mwenye umri wa miaka 29, alisema anatumaini tukio hilo lilikuwa la mara moja na halitajirudia tena. “Ndio ilikuwa ni jambo la kushangaza kidogo. Nilidhani mwanzo alikuwa anatania tu, lakini nikaona anaanza kunivuta nywele na kuanza kunitukana. Siku ile ya mechi nilizungumza na watu wengi na wote walionyesha kupendezwa na hiki ninachokifanya, lakini ghafla mtu mmoja akaja kuharibu kila kitu.
“Lengo langu mimi sio kuonyesha upungufu wa Man United. Daima mimi ni shabiki wa timu hii na nitaendelea kushirikiana na wenzangu katika nyakati ngumu na nzuri. Kusema kwamba sitanyoa nywele hadi tushinde mechi tano mfululizo kwa wakati ule sikuwa najua kama itadumu kwa muda mrefu kiasi hiki, nina matumaini tutakuwa na mfululizo mzuri wa ushindi hivi karibuni.
“Daima nitajitahidi kusambaza upendo na naamini hili lilikuwa ni tukio la mara moja tu.”