Shabiki Senegal afariki akienda uwanjani
Muktasari:
- Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) lilitoa rambirambi zake juzi jioni, likithibitisha tukio hilo la kusikitisha baada ya Senegal kushinda na kufuzu robo fainali, ikijiandaa kukabiliana na majirani zao wa Mali Ijumaa ya wiki hii.
TANGIER, MOROCCO: SHABIKI mmoja wa Senegal alifariki dunia katika ajali ya gari siku ya Jumamosi akiwa njiani kwenda Tangier ili kuishangilia timu ya Simba wa Teranga katika mechi ya 16 Bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 dhidi ya Sudan, ambapo wababe hao walipata ushindi wa mabao 3-1 na kutinga robo fainali.
Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) lilitoa rambirambi zake juzi jioni, likithibitisha tukio hilo la kusikitisha baada ya Senegal kushinda na kufuzu robo fainali, ikijiandaa kukabiliana na majirani zao wa Mali Ijumaa ya wiki hii.
“Shirikisho la Soka la Senegal limesikitishwa sana kutangaza kifo cha Aïda Faye Samb, kilichotokea kufuatia ajali ya barabarani katika barabara kuu ya Rabat–Kenitra,” FSF ilisema katika taarifa yake. Taarifa iliongeza: “Katika mazingira haya yenye maumivu makubwa, FSF inatoa pole za dhati kwa familia iliyofiwa, wapendwa wake, na familia nzima ya soka.”