Sh496 Billioni! Bei anayouzwa mtu hatari Haaland

MANCHESTER, ENGLAND. UNATAKA, Erling Haaland awe wako? Yale mabao anayopiga, awe anafanya hivyo akiwa kwenye kikosi chao? Basi ni rahisi tu, weka mkwanja wa Euro 200 milioni mezani.

Hata hivyo, pesa hiyo itaweza kumng'oa Haaland kutoka Etihad kuanzia 2025, kulingana na kipengele kilichochomekwa kwenye mkataba wake baada ya kunaswa na Manchester City akitokea Borussia Dortmund kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana.

Unaambiwa hivyo, Man City baada ya kumnasa Haaland na kumsainisha mkataba wa miaka mitano, walichomeka kipengele cha kumruhusu kwenda timu nyingine kama kutakuwa na kiasi fulani cha pesa kitalipwa. Kiasi hicho cha pesa kilichowekwa kwenye mkataba huo ni Euro 200 milioni. Lakini, kimewekewa muda pia, kwamba Haaland hataruhusiwa kuondoka kama kocha Pep Guardiola ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho cha Etihad.

Kwa maana kwamba, mwisho wa mkataba wa sasa wa Guardiola na Man City utakapofika tamati, kutakuwa na muda wa kusikilizia wa miezi 12 na baada ya hapo, ruksa kwa timu kuleta hiyo Euro 200 milioni ili kuvunja mkataba wa mkali Haaland huko Etihad.

Guardiola, mkataba wake wa awali ulikuwa unafika tamati mwishoni mwa msimu huu, lakini Novemba mwaka jana aliongeza miaka miwili ya kubaki Etihad, hivyo atakuwa kwenye benchi la mabingwa hao wa England hadi mwishoni mwa msimu wa 2024/25.

Imeelezwa hivi kuongezwa kwa mkataba wa Guardiola aendelee kubaki Man City kitendo hicho kimefanywa kwa ajili ya Haaland na hivyo kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake kinakwenda na hatima ya kocha huyo Mhispaniola.

Wakati Haaland anamwaga wino kusaini mkataba wa miaka mitano Man City, kwenye mkataba huo kuliwekwa kipengele cha kuvunjwa kinachohitaji Euro 200 milioni (Pauni 175.5milioni) na kwamba kingeenza kufanya kazi katikati ya muda wa mkataba wa mkali huyo.

Iliripotiwa kwamba kipengele hicho cha uwezekano wa kuvunja mkataba wa Haaland kingepaswa kufanya kazi mwishoni mwa msimu wa 2023/24 – ambao ni msimu wa pili wa Haaland Etihad.

Lakini, ripoti mpya inadai kwamba mkataba mpya aliopewa Guardiola utakaofika tamati 2025 utachelewesha kuanza kutumika kwa kipengele hicho kwenye mkataba wa Haaland kwa miezi 12 zaidi, hivyo kama Guardiola ataamua kuondoka Man City, Haaland naye itakuwa ruhusa kuondoka Etihad kama kutakuwa na timu itakayokuwa tayari kulipa mkwanja huo.

Taarifa ya Catalunya Radio iliyotolewa juzi Alhamisi, ambayo ilichambuliwa kwa kina zaidi na gazeti la Marca, ilibainisha kwamba mkataba wa Guardiola umeunganishwa moja kwa moja na kipengele cha kuvunja mkataba wa Haaland. Habari hiyo ni pigo kubwa kwa Real Madrid na Barcelona, ambazo zilikuwa zinafuatilia kwa karibu kipengele hicho kwenye mkataba wa Haaland.

Haaland alionyesha kiwango cha kibabe sana wakati Man City ilipoichapa RB Leipzig 7-0 Jumanne iliyopita katika mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Straika huyo alifunga mabao matano ndani ya dakika 35 na hat-trick yake alifunga kwenye kipindi cha kwanza, huku mabao hayo matano moja tu alilofunga kwa penalti.

Haaland sasa amefikisha na kuvuka mabao 30 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akifanya hivyo akiwa mchezaji kinda zaidi, umri wa miaka 22 na siku 236 - akivunja rekodi ya Kylian Mbappe kwa siku 116 - wakati alipofikisha mabao 30 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati Lionel Messi idadi hiyo ya mabao 30 alifikisha akiwa na umri wa miaka 23 na siku 131.