Semenyo ameshafanya uamuzi anakwenda wapi
Muktasari:
- Fowadi huyo wa Bournemouth amekuwa gumzo na kufukuziwa na timu nyingi kwenye Ligi Kuu England baada ya kuonyesha kiwango bora katika kikosi hicho cha pwani ya kusini.
LONDON, ENGLAND: WINGA, Antoine Semenyo ameshafanya uamuzi kwamba atakwenda kujiunga na Manchester City katika dirisha la usajili la Januari.
Fowadi huyo wa Bournemouth amekuwa gumzo na kufukuziwa na timu nyingi kwenye Ligi Kuu England baada ya kuonyesha kiwango bora katika kikosi hicho cha pwani ya kusini.
Semenyo, 25, alisaini mkataba mpya Julai mwaka huu, ambapo ulikuwa mpango wa Bournemouth wa kuzikata maini timu zilizokuwa zikihitaji saini yake kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Hata hivyo, kwenye mkataba huo mpya kuna kipengele kinachomruhusu Semenyo kuondoka mwaka 2026 endapo kama kutakuwa na timu itakayokuwa tayari kulipa ada ya uhamisho ya Pauni 65 milioni.
Klabu nyingi zimekuwa zikihitaji huduma ya staa huyo wa kimataifa wa Ghana ikiwamo Manchester United, Man City na Chelsea, ambayo hivi karibuni ilitangaza kujiondoa kwenye mchakamchaka huo. Lakini, ripoti zinafichua, Semenyo mwenyewe anataka kwenda kucheza chini ya kocha Pep Guardiola huko Etihad.
Man United ilipambana sana kunasa saini ya staa huyo, lakini kuna ugumu mkubwa wa dili hilo kukamilika. Hilo linatokana na ukweli kwamba mchezaji mwenyewe pia anasikiliziwa juu ya uamuzi na chaguo lake. Liverpool iliripotiwa pia kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo ambaye tayari ameshafunga mabao manane kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Kocha Guardiola alishasema huko nyuma kwamba Man City itafanya usajili kwenye dirisha la Januari. Bournemouth inaonekana imeshakubaliana na matokeo endapo kama itampoteza mshambuliaji huyo iliyemsajili kutoka Bristol City kwa ada ya Pauni 10 milioni mwaka 2023. Alipozungumza Jumanne iliyopita, kocha wa Bournemouth, Andoni Iraola alisema angependa sana kumbakiza Semenyo, lakini hana uwezo wa kuzuia kinaweza kutokea wakati dirisha litakapofunguliwa Januani Mosi.