Scholes ajielezea kwa Carrick kuhusu posti yake Insta
Muktasari:
- Kiungo huyo wa zamani wa mabingwa hao mara 20 wa England, Scholes aliandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii baada ya Man United kupoteza dhidi ya Newcastle United, Jumatano iliyopita. Ujumbe wake uliwashangaza mashabiki wengi.
MANCHESTER, ENGLAND: GWIJI wa Manchester United, Paul Scholes, amefunguka kuhusu ujumbe aliomtumia Michael Carrick baada ya chapisho lake la Instagram kuzua mjadala mkubwa wiki iliyopita.
Kiungo huyo wa zamani wa mabingwa hao mara 20 wa England, Scholes aliandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii baada ya Man United kupoteza dhidi ya Newcastle United, Jumatano iliyopita. Ujumbe wake uliwashangaza mashabiki wengi.
Scholes aliandika: “Michael ana kitu maalum sana ndani yake…Kwa sababu Utd wamekuwa wabaya katika mechi nne zilizopita… Usiku mwema! Tonali ❤️.”
Ujumbe huo mfupi uliwafanya mashabiki wengi kufikiri Scholes alikuwa akimshambulia Carrick kutokana na kushuka kwa kiwango cha timu katika mechi za karibuni.
Lakini, sasa Scholes ameeleza wazi hakumaanisha kumkosoa Carrick. Badala yake, alisema alikuwa akizungumza kuhusu ukweli timu imekuwa ikipata matokeo mazuri licha ya kucheza chini ya kiwango.
Akizungumza kwenye podikasti ya The Good, the Bad and the Football, Scholes alisema: “Haikuwa nia yangu kabisa kumkosea Michael.
Michael ni mmoja wa watu wazuri zaidi utakutana nao katika mpira wa miguu na yeye ndiye mtu wa mwisho ambaye ningependa kumkosea.”
Aliongeza kuwa alimwandikia Carrick moja kwa moja ili kufafanua: “Nilimtumia ujumbe mara moja nikisema ‘sikuwa na nia ya kukukasirisha’, ingawa sidhani kama hata ilikuwa lazima kufanya hivyo. Yeye mwenyewe aliniambia hakukasirishwa na jambo hilo. Nafikiri watu wamechukulia tofauti na maana halisi.”
Scholes aliendelea kueleza alimaanisha tu Man United haijacheza vizuri katika mechi nne zilizopita, lakini bado Carrick amekuwa akipata matokeo. Alirejea pia maneno ambayo mara nyingi yalitamkwa na meneja wa zamani wa Man United, Alex Ferguson: “Tulikuwa na meneja bora zaidi duniani na alikuwa akisema wakati mwingine unahitaji bahati kidogo. Hicho ndicho nilikuwa nasema.”
Carrick alianza kazi yake kama kocha wa Man United kwa ushindi kwenye mechi nne mfululizo, zikiwemo dhidi ya vinara wa ligi, Arsenal na wanaoshika nafasi ya pili Manchester City.
Licha ya Scholes kusema kiwango cha uchezaji kilishuka, kichapo dhidi ya Newcastle kilikuwa ni kipigo cha Carrick cha kwanza tangu aanze kuinoa timu katika mechi ya nane. Katika mechi nane za Man United chini ya Carrick, ameshinda sita, sare moja na kupoteza moja, ambapo alizichapa Arsenal, Man City, Fulham, Tottenham, Everton na Crystal Palace, huku aikitoka sare na West Ham United na kupoteza mbele ya Newcastle United, ambao ulikuwa mchezo wao wa mwisho.
Wakati baadhi ya nyota wa zamani wa Man United wamekuwa wakimkosoa Carrick, wengine wamemtetea. Beki wa kushoto wa zamani wa Man United, Patrice Evra, alisema haelewi kwa nini Carrick anakosolewa sana, aliposema: “Natumaini ile stori ya Instagram ya Scholes si ya kweli, natumaini akaunti yake ilidukuliwa.”
Aliongeza: “Kwa kweli sishangai sana. Akiwa mchezaji, Scholes alikuwa mtu mtulivu sana niliyewahi kucheza naye. Lakini, sasa kwenye vyombo vya habari anatoa kauli tata.”
Evra alisema pia haelewi kwa nini Carrick hapati uungwaji mkono wa kutosha, akisema amekuwa akifanya vizuri. Alikosoa pia uchambuzi hasi kutoka kwa magwiji wa Man United kama Roy Keane, Gary Neville na Scholes mwenyewe, ambao walipaswa kumuunga mkono mchezaji mwenzao huyo wa zamani ili kumpa moyo wa kufanya vizuri zaidi katika kikosi hicho cha Old Trafford.
Evra alisema: “Inanikera kwa sababu tunataka kuwa kwenye nne bora na maoni kama haya hayana ulazima. Lakini, hivi ndivyo inavyokuwa unapofanya kazi kwenye TV, huwezi kuwa chanya kila wakati, lazima uwe mkosoaji.”
Alimkumbusha pia Neville kuhusu uzoefu wake wa ukocha katika kikosi cha Valencia CF, akisema kwa utani: “Ni rahisi kuzungumza kwenye TV. Walipokuomba pilau, uliwapa samaki na chipsi.” Hiyo ilikuwa na maana Neville alishindwa kufanya vizuri kwenye ukocha wake katika kikosi cha Valencia na alifutwa kazi baada ya siku chache tu.
Evra alihitimisha kwa kusema ingawa wachezaji hao ni magwiji wa klabu kama wachezaji, hawajafanikiwa sana kama makocha na kutuma ujumbe kwao kimtindo, aliposema: “Kwa hiyo kusema mambo ambayo yanaweza kuharibu kazi ya kocha mwingine ni kupita kiasi kidogo.”
MECHI ZIJAZO ZA MAN UNITED
-Machi 15 vs Aston Villa (nyumbani)
-Machi 20 vs Bournemouth (ugenini)
-Aprili 13 vs Leeds United (nyumbani)
-Aprili 18 vs Chelsea (ugenini)
-Aprili 27 vs Brentford (nyumbani)