Sababu Onana kupaka mafuta gloves, mbinu nyingine za mastaa uwanjani

Muktasari:

  • Wapo pia wanaovaa kofia kujikinga na jua hasa makipa, wengine wanavaa maski kama Victor Osimhen ili kuzui asipate majeraha eneo la taya ambalo aliwahi kuumia, plasta vidoleni huku wengine wakifanya hivyo kwa lengo la kuzuia pete zao za ndoa kuonekana au kutokuleta madahara kwa wenzao kwa sababu haziruhusiwi na hawataki kuzitoa vidoleni.

LONDON, ENGLAND: Katika mchezo wa soka, wachezaji wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za kuwafanya wafanye vizuri, wapo wanaochagua aina ya viatu vya kuchezea, wanaotoboa soksi na wanaopaka mafuta mwilini kwa lengo la kuwafanya wapinzani wanaopenda kuwashika wasifanikiwe.

Wapo pia wanaovaa kofia kujikinga na jua hasa makipa, wengine wanavaa maski kama Victor Osimhen ili kuzui asipate majeraha eneo la taya ambalo aliwahi kuumia, plasta vidoleni huku wengine wakifanya hivyo kwa lengo la kuzuia pete zao za ndoa kuonekana au kutokuleta madahara kwa wenzao kwa sababu haziruhusiwi na hawataki kuzitoa vidoleni.

Hata hivyo, mbali na mbinu hizo na nyingine nyingi ambazo zimekuwa ikitumiwa na mastaa wengi, kuna hii ya kupaka mafuta kwenye glovu za makipa.

Katika mchezo wa Ligi Kuu England wa Manchester United dhidi ya Liverpool siku za hivi karibuni, kipa Andre Onana alionekana akipaka kiasi kikubwa cha mafuta aina ya Vaseline kwenye glovu zake wakati fulani Liverpool ilipokuwa imeenda kupiga kona.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye dimba la Old Trafford na kumalizika kwa sare ya bao 2-2, mashabiki wengi walionekana kushangazwa na kitendo hicho ingawa kipa wa zamani wa Man United  Mark Bosnich alikuja na ufafanuzi kwanini Onana alifanya hivyo.

Bosnich aliiambia Sky Sports: “Kitu pekee ninachoweza kusema inasaidia kudaka na kuushika mpira vizuri. Makipa wengi wanapenda glavu zao zilowe kidogo kwa sababu raba nyembamba inayokuwa kwenye kiganja huwa ngumu kiasi cha kukufanya upate tabu kuushika mpira kwani huteleza.

Mbali ya Bosnich, baadhi ya makipa wengine kama Shay Given na Ben Foster wamefunguka ni kweli mafuta aina ya Vaseline yanasaidia kuushika mpira vizuri na hata wao walishawahi kutumia.

“Nakumbuka kwa mara ya kwanza nilimwona Joe Hart akipaka Vaseline katika mashindano ya Kombe la Dunia kule Brazil mwaka 2014, alipaka kwenye glovu zake tulipokuwa mazoezini na kuniambia inasaidia,” alisema Foster.

Hata hivyo, Vaseline ni moja ya njia tu ambazo wachezaji huzitumia katika kurahisisha kazi zao, hapa zipo njia nyingine tano ikiwa pamoja na kutoboa soski zinazotumiwa na mastaa mbalimbali duniani kurahisisha na kuongeza ufanisi wa kazi zao.

WANAOTOBOA SOSKI

Beki wa Manchester City, Kyle Walker mara kadhaa ameonekana akicheza huku soksi zake zikiwa na matobo mengi ya umbo la duara hususani kwenye vigimbi.

Walker anatajwa ni mmoja kati ya mastaa wa mwazo katika EPL kuvaa soksi zenye mwonekanao huo na alionekana nazo kwa mara ya kwanza mwaka 2018 katika mechi ya ngao ya hisani dhidi ya Chelsea.

Sababu ya mashimo hayo nyuma ya soksi ni kuzuia uwezekano wa kubanwa kwa misuli na kusababisha damu isitembee kwa uhuru hali inayoweza kuchangia maumivu ya misuli kwa damu kushinda kutiririka vizuri.

Mchezaji mwenzake wa Man City, Jack Grealish amekuwa akitumia njia ya kushusha soksi zake chini kabisa wakati anacheza kama njia moja wapo ya kukabiliana na hilo. Mastaa wengine wamekuwa wakizikata soksi kwa chini kisha kuvaa soksi zao ambazo wanaona hazitowaumiza misuli.


KUJIPAKA MAFUTA MWILINI

Wakati fulani, mchezaji wa zamani wa Wolves, Adama Traore alionekana akijipaka mafuta mikononi kuanzia viganjani hadi karibu na mabega.

Tukio hili lilikuwa linazua sana mjadala katika mitandao ya kijamiii na kocha wake wa wakato huo Nuno Espirito Santo alipoulizwa sababu ya Traore kufanya hivyo akajibu inamsaidia mabeki wanaotaka kumshika washindwe kufanya hivyo kwani atakuwa anateleza na zaidi ni kwa sababu alikuwa na shida kwenye bega lake.

“Ni wazo zuri sana ambalo lilibuniwa na idara ya matibabu na hiyo ni kwa sababu ni majeraha aliyoyapata kwenye bega lake,” alisema  Nuno mwaka 2021.

“Kwa sababu kama wachezaji wakimshika mkono wake wanatengeneza hatari ya kumrudisha tena katika majeraha ya bega, tangu atumie mafuta hayo inakuwa ni ngumu sana kumzuia Traore.”

PLASTA za MAPAJA, MIGUU

Gareth Bale akiwa Real Madrid aliwahi kuonekana akiwa na plasta aina ya neon adhesive physio tape kwenye mapaja yake, baada ya hapo Cristiano Ronaldo naye akaonekana nazo.

Wachezaji wengi duniani wakashawishika kuvaa plasta hizo zenye rangi ya bluu ambazo kazi yake kubwa ni kusaidia misuli kutokukaza.

KUJICHORA MACHO

Mastraika walikuwa na wakati mgumu sana walipokutana na kipa wa kimataifa wa Uturuki Rustu Recber ambaye aliwahi kuzichezea Barcelona na Fenerbahce.

Alichukua mbinu hii kutoka katika mchezo wa Rugby na muda wote alipokuwa uwanjani ungemwona na mistari chini ya macho yake kama ile wanayijichora wanajeshi wanapokuwa katika mapambano.

Inaelezwa michoro hiyo ilikuwa ikimsaidia kupunguza ukali wa mwanga uliokuwa unammulika. Haikujulikana ikiwa kuna athari yoyote aliyokutana nayo kwa kupata unga huo.