Rosicky ataka ubosi Arsenal
Muktasari:
- Rosicky, 44, ni rafiki wa karibu wa kocha wa sasa wa Arsenal, Mikel Arteta na bosi wa akademia ya klabu hiyo, Per Mertesacker.
LONDON, ENGLAND: STAA wa zamani wa Arsenal, Tomas Rosicky anaripotiwa kuwa kinara kwenye mbio za kufukuzia nafasi ya kuwa mkurugenzi mpya wa michezo wa timu hiyo.
Rosicky, 44, ni rafiki wa karibu wa kocha wa sasa wa Arsenal, Mikel Arteta na bosi wa akademia ya klabu hiyo, Per Mertesacker.
Rosicky aliitumikia Arsenal kwa miaka 10, wakati alipokuwa akicheza sambamba na Arteta na Mertesacker.
Arsenal kwa sasa ipo sokoni kusaka mtu wa kuja kuchukua mikoba ya Edu tangu alipoondoka kwenda kuungana na bilionea mmiliki wa klabu ya Nottingham Forest, Evangelos Marinakis kwenye klabu zake, Novemba mwaka jana.
Edu, ambaye pia alikuwa mchezaji wa zamani wa Arsenal, aliajiriwa mwaka 2019 kama mkurugenzi wa ufundi kabla ya kuwa mkurugenzi wa michezo 2022.
Lakini, Rosicky anataka kuheshimu mkataba wake huko Sparta Prague, ambao utafika tamati mwishoni mwa msimu.
Rosicky alichukua majukumu ya kuwa mkurugenzi wa michezo kwenye klabu hiyo ya Sparta Prague, Desemba 2018, mwaka mmoja baada ya kustaafu soka.
Klabu hiyo ya Jamhuri ya Czech ilifuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu chini yake na mwaka jana ilishinda taji lake la kwanza tangu mwaka 2013.
Sparta, ambayo Rosicky aliichezea kwenye zama mbili tofauti - ameiongoza timu kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Czech huku timu hiyo kwa sasa ikiwaongoza wapinzani wao wakubwa Slavia Prague kwa tofauti ya pointi 13.
Aliyekuwa makamu wa Edu, Jason Ayto, kwa sasa ndiye anayesimamia kazi za mkurugenzi wa michezo huo Arsenal tangu Mbrazili huyo alipoondoka, Novemba mwaka jana na ataiongoza timu hiyo kwenye dirisha hili la usajili wa Januari.