Rooney aishauri Arsenal kucheza kibabe kuizuia Man City
Muktasari:
- Kwa sasa Arsenal wanaongoza msimamo wakiwa na pointi 70 wakifuatiwa na City wenye pointi 61, lakini wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
LONDON, ENGLAND: GWIJI wa Ligi Kuu England na Manchester United, Wayne Rooney amewashauri wachezaji wa Arsenal 'kucheza kwa nguvu na kibabe' ili waweze kuifunga Manchester City katika pambano muhimu la ubingwa wa Ligi Kuu England litakalopigwa Aprili 19, mwaka huu.
Rooney, ambaye ni mmoja wa wafungaji bora wa muda wote wa Manchester United, alitoa maoni hayo wakati ligi ikiingia hatua za mwisho ambapo kila pointi ina umuhimu mkubwa.
Kwa sasa Arsenal wanaongoza msimamo wakiwa na pointi 70 wakifuatiwa na City wenye pointi 61, lakini wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
Ushindi kwa Gunners katika mchezo ujao unaweza kuwasogeza kwenye ubingwa, huku ikiwa City itaibuka na ushindi utafufua ushindani.
Akizungumza kabla ya mechi hiyo itakayopigwa katika Uwanja wa Etihad, Rooney alisema timu ya Pep Guardiola ina faida za kisaikolojia. Nadhani City wana faida kidogo kutokana na kocha na wachezaji walionao. Wataweza kubaki watulivu zaidi kuliko Arsenal. Arsenal wanaweza kuwa na wasiwasi, hasa unapopoteza mechi chache mfululizo unaanza kujiuliza ushindi ujao utatoka wapi. Mawazo hasi yanaathiri sana kiwango chako,” alisema Rooney.
Kutokana na uzoefu wa Man City katika kushughulikia presha, Rooney alishauri kuwa kocha Mikel Arteta na vijana wake wa Arsenal wanapaswa kucheza kwa nguvu na kibabe na sio kufeki ili kuwafanya City wapate ugumu kupata matokeo mazuri.
“Haijalishi mashabiki wanapenda aina hiyo ya mchezo au la, wanapaswa kufanya kila liwezekanalo kuizuia City kushinda. Wanahitaji kuwa imara vya kutosha kuwazuia kufunga,” aliongeza.