Ronaldinho alivyoachana na De Lima njia panda

HIVI karibuni ziliibuka stori za mchezaji wa zamani wa Barcelona, PSG, AC Milan na timu ya taifa ya Brazil, Ronaldhino Gaucho, 44, ikieleza kwamba hali yake ya kiuchumi inazidi kuwa mbaya.

Hii sio mara ya kwanza kwa kiumbe huyo aliyewahi kupigiwa makofi na mashabiki wa Real Madrid katika uwanja wa Santiago Bernabeu licha ya kwamba alikuwa akiichezea Barcelona. Hiyo ilitokana na kipaji kikubwa alichojaaliwa kuwa nacho.

Katika ubora wake kwenye miaka ya 2004 hadi 2007, kila mtu aliyeupenda mpira wa miguu alitamani kumuona akiwa uwanjani, haijalishi amevaa jezi ya timu aliyoipenda au la ilikuwa ni raha tu kumuangalia Ronaldinho akicheza soka.

Tuzo ya Ballon d’or 2005 ikaenda kwake. Ni kama mpira ulizaliwa kwa sababu yake na yeye alizaliwa kwa sababu ya mpira, lakini baada ya yote hayo maisha sasa yamebadilika.

Kwa sasa madeni na umaskini ni sehemu ya maisha yake. Mwaka jana ripoti za The Sun zilieleza kwamba alikuwa akidaiwa zaidi ya Euro 2 milioni na mamlaka za kodi nchini Brazil ambapo baada ya kuingia akaunti yake ili kuchukua pesa hizo walikuta ana Dola sita pekee.

Baada ya kuona hivyo wakaamua kuchukua mali zake ikiwemo nyumba na magari aliyokuwa anamiliki ili wauze na kulipa deni hilo. Huyo ndiye Ronaldinho.

Stori yake ni tofauti, sio kama hakuwekeza kama ilivyo kwa wachezaji wengine wa Kibrazili, hapana. Kwa mujibu wa tovuti ya Allfootball jamaa ana nyumba zisizopungua 50 huko Brazil. Mwaka 2017 alisaini mkataba wa kuwa balozi wa Barcelona kwa miaka 10. Mwaka uliofuatia akasaini dili jingine na kampuni ya World Soccer Coin (WSC) kuwa balozi wao.

Mwaka 2017, aliingia makubaliano na mfanyabiashara kutoka Italia, Fabio Cordella kutumia jina lake kwenye kampuni yake iitwayo ‘wine of Champions’ ambayo inatengeneza vinywaji vya aina 11 tofauti. Lakini yote hajamsaidia.

Mwaka 2020 alikamatwa nchini Paraguay kwa kosa la kuingia ha pasipoti feki. Akatakiwa kulipa faini ya zaidi ya Dola 90,000.

Lakini si hivyo tu mikasa ni sehemu ya maisha yake, kwani aliyekuwa mchumba wake, Priscilla Coelho alifungua kesi ya kudai mgawo wa mali 2019 muda mfupi baada ya kuachana.

Ronaldinho maisha yake hajawahi kuwa sawa. Amekuwa mtu wa kutangatanga, huku kila uchao pesa zikizidi kumkimbia.

Hiyo imekuwa ni tofauti na mmoja kati ya washkaji wa kizazi chake, Ronaldo de Lima ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 47. Kwa mujibu wa mtandao wa Goal.com ana utajiri unaofikia Dola 300 milioni.

Achana na hiyo kwa sasa ndiye mmiliki wa Real Valladolid inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza  Hispania.

De Lima ana hisa katika timu ya mchezo wa raga iitwayo Fort Lauderdale ya Marekani na hajaishia  hapo pia ni mmiliki mwenza wa timu ya mashindano ya magari ya A1 Team Brazil.

Kampuni yake ya Agency 9ine ndio inamsimamia Neymar na wachezaji wengine wengi wa michezo mbalimbali.

De Lima maisha yake ni tofauti kabisa na Ronaldinho, kwani tangu alipostaafu soka hajawahi kuhusika katika kesi yoyote ambayo ingesababisa akamatwe na polisi.

Mwanzo Ronaldinho alichagua njia sawa na De Lima yaani kucheza soka kwani naye kacheza timu kubwa, lakini wakaachana njia panda kwa maana ya namna walivyotuliza akili, kuwekeza na kutumia utajiri wao kwa akili.

De Lima alicheza Cruzeiro, PSV, Barcelona, Inter Mila, Real Madrid, AC Milan na Corithians.

Wakati Ronaldinho anaamini fedha alizopata zingetosha kumfanya aishi kifahari siku zote, De Lima alikuwa bize kupata kikubwa zaidi za hicho. Aliwekeza na kuanzisha biashara mbalimbali.

Wote walikuwa na njia moja wakati wanacheza kuanzia umaarufu na pesa walizokuwa wanazipata na Ronaldinho kuna wakati alikuwa akipata zaidi, mfano mwaka 2006 alikunja zaidi ya Dola 16 milioni kutokana na mikataba ya ubalozi.

Lakini, Ronaldo alikuwa mjanja zaidi jinsi alivyomaliza mwisho wa muvi. Wakati Ronaldinho anafikiria episodi moja, De Lima alifikia sizoni. Hapa ndipo walipoachana, huyu alienda kulia kisha yule akaenda kushoto.