Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rio Ferdinand aipa ujanja Manchester United

RIO Pict

Muktasari:

  • United kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na mechi saba mkononi, ikipambana kuhakikisha inapata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

MANCHESTER, ENGLAND: NGULI wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand, ameishauri klabu hiyo kuweka nguvu kubwa katika usajili wa viungo wawili kwenye dirisha lijalo la majira ya joto, akisisitiza pia kuongeza wachezaji katika nafasi nyingine mbili muhimu.

United kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na mechi saba mkononi, ikipambana kuhakikisha inapata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Mafanikio hayo yamekuja baada ya kuimarika kwa kiwango chao chini ya kocha wa muda, Michael Carrick, ambaye ameiongoza kushinda mechi saba na kupoteza moja tu tangu alipochukua mikoba ya ufundi.

Hata hivyo, bado haijaamuliwa kama Carrick atapewa mkataba wa kudumu kuinoa timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford.

Akizungumza kwenye kipindi chake, Ferdinand amesema United wanahitaji kufanya usajili wenye tija badala ya kubadilisha kikosi kizima.

“Iwapo watasajili wachezaji wanne na wawili kati yao wakawa wa kikosi cha kwanza, huo utakuwa usajili mzuri na wa uhalisia,” amesema Ferdinand.

Alifafanua kipaumbele chake kingekuwa kusajili viungo wawili wa kati, mmoja wa kuanza na mwingine kijana wa kukuza ili kuongeza ushindani sambamba na Bruno Fernandes na Kobbie Mainoo.

Pia, Ferdinand alipendekeza kusajili mshambuliaji kijana wa kuongeza nguvu pamoja na beki wa pembeni ili kuimarisha safu ya beki.

Katika tetesi za usajili, United imehusishwa na kiungo wa Newcastle United, Sandro Tonali, huku ripoti zikidai klabu hiyo inaweza kulazimika kuuza nyota wake iwapo itashindwa kumaliza ndani ya nafasi tano bora kutokana na masharti ya kifedha.

Hata hivyo, Ferdinand anaamini chaguo bora zaidi kwa sasa ni kiungo wa Nottingham Forest, Elliot Anderson, ambaye amekuwa katika kiwango kizuri.

“Elliot Anderson anaonekana kuwa chaguo sahihi. Ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa, ana nguvu, anafanya kazi nyingi uwanjani na anaweza kuisukuma timu mbele,” aliongeza.

Aidha, aligusia kushuka kwa kiwango kwa Carlos Baleba ambaye alikuwa akitajwa sana mwanzoni mwa msimu, huku akibainisha bado kuna vipaji vingine ambavyo vinaweza kuibuliwa.

Kwa mtazamo wa Ferdinand, United hawahitaji mageuzi makubwa, bali usajili makini wa wachezaji wachache wenye ubora ili kurejesha makali ya timu hiyo kongwe England.