Refa wa Man United ameonyeshwa picha sio
Muktasari:
- Everton ilinyima penalti kwenye dakika za majeruhi kwa uamuzi wa utata wa VAR. Staa wa Everton, Ashley Young alianguka ndani ya boksi baada ya kuvutwa jezi na Matthijs De Ligt, tukio ambalo lilimfanya mwamuzi wa mchezo huo, Andy Madley kutoa adhabu ya mkwaju wa penalti.
MANCHESTER, ENGLAND: REFA wa zamani wa Ligi Kuu England, Mark Halsey ameishambulia VAR akisema ni ya hovyo baada ya kuinyima Everton nafasi ya kushinda mechi kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Manchester United uwanjani Goodison Park, jana Jumamosi.
Everton ilinyima penalti kwenye dakika za majeruhi kwa uamuzi wa utata wa VAR. Staa wa Everton, Ashley Young alianguka ndani ya boksi baada ya kuvutwa jezi na Matthijs De Ligt, tukio ambalo lilimfanya mwamuzi wa mchezo huo, Andy Madley kutoa adhabu ya mkwaju wa penalti.
Mwamuzi aliyekuwa kwenye VAR, Matt Donohue alimtaka Madley kwenye kujihakikishia uamuzi wake kwa kwenda kuangalia marudio ya tikio hilo kwenye skrini ya VAR iliyokuwa uwanjani hapo - ambako alikwenda kuonyeshwa picha tofauti kabisa zilizomfanya afute uamuzi wa kuipa Everton penalti waliyostahili.
Mwamuzi mstaafu Halsey alisema: "Uamuzi wa kubadili penalti waliyopewa Everton na kufanya mechi yao na Manchester United kumalizika kwa sare ya 2-2 yalikuwa makosa makubwa.
"Refa wa VAR, Matt Donohue hakupaswa kuingilia uamuzi huo kwa sababu mwamuzi Andy Madley, aliyekuwa uwanjani aliona wazi kabisa kwamba kulikuwa na kosa. Ashley Young alivutwa jezi - na beki wa timu pinzani anapofanya hivyo ndani ya boksi anajitafutia matatizo.
"Na Madley alipokwenda kwenye skrini ya VAR uwanjani hapo, alionyeshwa picha tofauti. Baadaye Ligi Kuu England iliposti kwenye mitandao ya kijamii kwamba tukio la Harry Maguire alilocheza dhidi ya Young limetazamwa kwa umakini na ilionekana hakukuwa na faulo yoyote iliyofanyika.
"Lakini, walishindwa kulifikiria suala la Matthijs de Ligt kumvuta jezi Young. Refa Madley angeonyeshwa picha zilizpiga nyuma ya goli angeliona hilo. Tukio hilo ni aibu kubwa."
Everton iliongoza 2-0 hadi mapumziko, shukrani kwa mabao ya Beto na Abdoulaye Doucoure. Lakini, Man United ilipambana kipindi cha pili na kufunga kupitia kwa Bruno Fernandes na Manuel Ugarte kupata sare.
Kocha wa Man United, Ruben Amorim alipoulizwa kuhusu penalti hiyo, alisema: "Hapana, nadhani ilikuwa nyepesi sana, haikuwa penalti kwa nilichokiona. Nadhani ingekuwa penalti nyepesi sana, hilo lipo wazi."
Lakini, kocha wa Everton, David Moyes kwa hasira alisema: "Siwaelewi kabisa. De Ligt alivuta jezi."