Marekani yataja sababu refa Msomalia kuzuiwa
Muktasari:
- Mnamo Juni 6, Artan aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami akitokea Uwanja wa Ndege wa Istanbul.
Msemaji wa Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani (CBP), amethibitisha kuwa mwamuzi wa Somalia, Omar Abdulkadir Artan, alizuiwa kuingia nchini humo kutokana na wasiwasi unaohusiana na masuala ya usalama.
Mnamo Juni 6, Artan aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami akitokea Uwanja wa Ndege wa Istanbul.
Wakati wa mchakato wa kuingia Marekani, refa huyo alifanyiwa ukaguzi wa ziada, ambao ni utaratibu wa kawaida unaotumiwa na idara hiyo pale maafisa wanapohitaji kuthibitisha taarifa au kubaini kama mtu anaruhusiwa kuingia nchini.
Baada ya ukaguzi kukamilika, ilibainika kuwa msafiri huyo, ambaye ni mwamuzi wa Kombe la Dunia, hakuruhusiwa kuingia Marekani kutokana na masuala ya uhakiki wa usalama, hivyo akanyimwa ruhusa ya kuingia nchini humo.
"Wasafiri wote wanaotaka kuingia Marekani, wakiwemo wanamichezo, makocha na maafisa wa kiufundi, hufanyiwa ukaguzi na uchunguzi na Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka.
"Maamuzi ya kuruhusu au kutoruhusu mtu kuingia nchini hufanywa kwa kuzingatia kila kesi kivyake, kwa kutumia taarifa zilizopo kutoka vyombo vya sheria, usalama wa taifa na uhamiaji wakati wa ukaguzi.
"Maofisa wa CBP pia wana mamlaka ya kuwahoji wasafiri, kufanya upekuzi na kuamua iwapo mtu apewe au anyimwe ruhusa ya kuingia nchini kwa mujibu wa sheria za Marekani," imesema taarifa ya CBP.