Redick ana taji la Lakers NBA?
Muktasari:
- Redick mwenye umri wa miaka 41 aliiongoza Lakers msimu uliopita katika safari yake ya kwanza kama kocha, akimaliza na rekodi ya ushindi wa mechi 50 na kupoteza 32.
CALIFORNIA, MAREKANI: LOS Angeles Lakers imeweka msimamo kuhusu mustakabali baada ya kumpa kocha mkuu Jonathan Clay Redick maarufu kama JJ Redick mkataba mpya wa kuendelea kuinoa timu hiyo, jambo linaloongeza hamasa kuelekea msimu wa 2025/26.
Redick mwenye umri wa miaka 41 aliiongoza Lakers msimu uliopita katika safari yake ya kwanza kama kocha, akimaliza na rekodi ya ushindi wa mechi 50 na kupoteza 32.
Timu hiyo ilishika nafasi ya tatu katika ukanda wa Magharibi, ingawa safari yao ilikatishwa mapema kwenye hatua ya kwanza ya mtoano dhidi ya Minnesota Timberwolves.
Meneja wa Lakers, Rob Pelinka ndiye aliyetangaza habari za mkataba mpya wa Redick katika mkutano na wanahabari uliofanyika mjini El Segundo, California akisema kocha huyo atakuwapo msimu ujao akianza mapema tu kukiwasha.
“Siichukulii kawaida nafasi hii. Najua ni nadra kocha anayeanza kazi yake kupata mkataba wa kuongezewa mapema, lakini nimebarikiwa kuwa sehemu ya taasisi inayoniamini,” anasema Redick.
NAFASI YA DONCIC
Katika hatua nyingine kubwa lilioshitua ni Luka Doncic aliyeshtua wengi alipohamia Lakers Februari, mwaka huu, katika moja ya uhamisho ghali zaidi katika historia ya NBA akisaini mkataba wa nyongeza wa miaka mitatu wenye thamani ya Dola 165 milioni mwezi Agosti. Hii inamuweka katika mstari wa mbele kama nguzo ya kikosi kwa sasa.
Doncic mwenye umri wa miaka 26 ametumia likizo yake ya kiangazi kuimarisha kiwango chake katika mashindano ya EuroBasket akiwa na Slovenia, alikoonekana kuwa na mwanga mpya akimshawishi Redick kuwa amejiandaa kwa safari ndefu.
“Nimezungumza naye mara nyingi. Tumekutana hapa na hata Las Vegas kwenye tamasha la muziki. Niliona ameweka maisha yake yote kwenye kazi hii. Amejenga utaratibu mpya wa kila siku na nimejiandaa kumuona Luka bora zaidi,” anasema Redick.
Kuongezwa kwa mchezaji wa kati DeAndre Ayton kwa mkataba wa miaka miwili kunampa Doncic mtu wa kusaidiana naye, huku ujio wa Marcus Smart ukiongeza uzoefu kwenye kikosi hicho.
LEBRON BADO YUMO
Hata hivyo, mjadala mkubwa unabaki kwa LeBron James ambaye akiwa na umri wa miaka 40, anajiandaa kuanza msimu wa 23 NBA.
“Kwanza kabisa tunamheshimu LeBron kwa kila kitu alichofanya. Ana haki ya kuamua mwisho wake mwenyewe akiwa na familia yake. Lakini tungependa sana kuona anastaafu akiwa Lakers,” anasema Pelinka.
Redick pia alikutana na LeBron mara mbili wakati huu wa likizo ikiwemo pia nyakati walipozungumza huko New York na Los Angeles. Kocha huyo alionekana kufurahishwa na hali ya mchezaji huyo ambaye msimu uliopita alikuwa na wastani wa pointi 24.4 kwa mechi. “Niliondoka nikiwa na uhakika yupo tayari. LeBron bado ni mfano wa kuigwa,†anasema Redick.
PRESHA KWA LAKERS
Licha ya mashaka juu ya mustakabali wa LeBron, Lakers wanaingia msimu huu wakiwa na matarajio makubwa kama kawaida.
Redick hakusita kukiri kuwa presha ya kuchukua ubingwa ni kubwa kila mwaka. “Kila siku ukiingia kwenye jengo hili unakumbushwa kuhusu historia ya Lakers na kiwango cha ubora kilichowekwa. Hivyo presha ipo. Haibadiliki,” anasema.
Kwa sasa, Lakers wana uhuru wa kufanya maboresho ya kikosi msimu ukiendelea, lakini Pelinka anadai hawatakimbilia kuyafanya kabla ya mechi 20 za kwanza kumalizika. Hii inawapa nafasi Redick na nyota wake kuwa na muunganiko mzuri wa kikosi chenye lengo la kurejesha ubingwa wa NBA jijini Los Angeles.