Raya abeba tuzo ya kipa bora EPL

Muktasari:

  • Raya ambaye amejiunga na Arsenal Oktoba mwaka jana kwa mkataba wa mkopo wa msimu mmoja uliokuwa na ada ya uhamisho ya Euro 3.5 milioni amekuwa kipa tegemeo sana ndani ya kikosi cha Arsenal msimu huu akichukua nafasi ya Aaron Ramsdale ambaye muda mwingi anasugua benchi.

LONDON, ENGLAND: KIPA wa Arsenal anayewatumikia kwa mkopo akitokea Brentford, David Raya ameshinda Tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya kucheza mechi 15 bila ya kuruhusu bao.

Raya ambaye amejiunga na Arsenal Oktoba mwaka jana kwa mkataba wa mkopo wa msimu mmoja uliokuwa na ada ya uhamisho ya Euro 3.5 milioni amekuwa kipa tegemeo sana ndani ya kikosi cha Arsenal msimu huu akichukua nafasi ya Aaron Ramsdale ambaye muda mwingi anasugua benchi.

Kucheza mechi 15 bila ya kuruhusu bao ndani ya EPL msimu huu kumempa tuzo hiyo kwa sababu mpinzani wake wa karibu Jordan Pickford wa Everton amecheza mechi 12 bila ya kuruhusu nyavu kutikisika na zimebaki mechi mbili hivyo hata kama atazuia hadi msimu unamalizika hatoweza kumfikia Raya.

Katika mechi 15 ambazo Raya alimaliza bila ya kuruhusu bao, 10 kati ya hizo alizipata tangu kuanza kwa mwaka huu ambapo amecheza mechi 15 na kuzuia 10.

Mbali ya kumaliza mechi nyingi bila ya kuruhusu bao kwa upande wa EPL, Raya pia alifanikiwa kutoruhusu nyavu zake zitikiswe katika mechi nne kati ya tisa za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Mkataba wa kipa huyu na Brentford unamalizika mwakani na Arsenal imeripotiwa kuwa katika mazungumzo ya kumsajili mazima.