Raphinha, Fermin mtegoni Barcelona
Muktasari:
- Kauli zake zinaelezwa kwamba huenda zikamfanya ajikute kwenye uchunguzi wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), kutokana na kupiga uamuzi wa waamuzi ambao wamewekewa kinga ya kutoshambuliwa na wachezaji, makocha na viongozi wa klabu ili kuwezesha uhuru wao kitaaluma uheshimike.
MADRID, HISPANIA: INGAWA hakupata hata dakika moja ya kucheza, kiungo wa Barcelona, Raphinha Dias alikuwa miongoni mwa wakosoaji wakubwa baada ya chama lake kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Atletico Madrid, akitoa lawama kuhusu uamuzi wa waamuzi.
Kauli zake zinaelezwa kwamba huenda zikamfanya ajikute kwenye uchunguzi wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), kutokana na kupiga uamuzi wa waamuzi ambao wamewekewa kinga ya kutoshambuliwa na wachezaji, makocha na viongozi wa klabu ili kuwezesha uhuru wao kitaaluma uheshimike.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil aliyekuwa nje kutokana na majeraha, alisafiri hadi Madrid kushuhudia kipigo cha Barcelona katika Uwanja wa Metropolitano kwenye mechi robo fainali. Barcelona ilitolewa kwa jumla ya mabao 3-2, licha ya kushinda mchezo wa pili kwa mabao 2-1.
Kikosi hicho cha Hansi Flick kilionyesha moyo wa kupambana kupitia mabao ya Lamine Yamal na Ferran Torres yaliyosawazisha matokeo ya jumla, lakini bao la ushindi kutoka kwa Ademola Lookman liliihakikisha Atlético Madrid kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Pigo la mwisho lilikuja baada ya beki Eric García kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia kumchezea vibaya Alexander Sorloth, tukio lililomkasirisha Raphinha aliyekuwa akiwashambulia waamuzi wakati mechi inaendelea.
“Ilikuwa ni wizi mtupu. Mwamuzi alikuwa na matatizo mengi. Kulikuwa na uamuzi wa ajabu sana. Sijui ni faulo ngapi Atletico Madrid walifanya bila kuonyeshwa kadi,” alilalamika hadharani mchezaji huyo.
Barcelona pia walidai walipaswa kupewa penalti baada ya Dani Olmo kuchezewa vibaya kipindi cha kwanza, tukio lingine lililochochea mjadala kuhusu uamuzi wa waamuzi, ingawa Raphinha hakutaka kulizungumzia.
Huo ni mchezo wa pili mfululizo ambao klabu hiyo imekuwa ikilalamikia uamuzi wa waamuzi katika Ligi ya Mabingwa, baada ya Uefa hivi karibuni kukataa malalamiko yao rasmi kuhusu uamuzi wa mechi iliyotangulia.
“Ni kawaida kwa binadamu kukosea, lakini kurudia tena…” Raphinha alisisitiza. “Tulicheza vizuri sana, lakini walituondolea nafasi ya kusonga mbele. Inaonekana tunapaswa kufanya kazi mara tatu zaidi ili kushinda.”
Katika hatua nyingine, kiungo wa timu hiyo Fermin Lopez alijikuta akivuja damu nyingi baada ya kupigwa teke usoni wakati wa mchezo.
Lopez, mwenye umri wa miaka 22, alishika uso huku damu ikimwagika baada ya kugongwa bahati mbaya puani na soli za viatu vya kipa wa Atletico Madrid, Juan Musso. Hata hivyo, cha kushangaza ni kwamba mchezaji huyo wa kimatifa wa Hispania alirejea uwanjani ndani ya dakika chache akiwa safi kana kwamba hakuna kilichotokea, licha ya tukio hilo la kutisha.
Ingawa mashabiki mitandaoni walimsifu kwa ujasiri wake, huku mmoja akieleza kuwa ana “roho ya kufa kwa ajili ya Barcelona”, lakini huenda akalazimika kutumia siku mbili hadi tatu akiwa nje kujiuguza kwani uwanjani alipewa huduma ya dharura tu ambayo baadaye huenda maumivu yalitarajiwa kuanza na huenda akawa na mchaniko kichwani kwa ndani. Mechi nyingi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya zilipigwa jana, ambapo Arsenal iliikaribisha Sporting CP huku Bayern Munich ikiwaalika Real Madrid kwenye Uwanja wa Allianz Arena mjini Munich.