Pogba ndo hivyo tena

Muktasari:
- Pogba, 30, alifanyiwa vipimo vya dawa aina ya DHEA Agosti mwaka jana, ambazo huongeza kiwango kikubwa cha homoni aina za testosterone.
Turin, Itala. Aliyekuwa kiungo Manchester United, Mfaransa Paul Pogba amefungiwa kujihusisha na soka kwa miaka minne baada ya kukutwa na hatia ya kutumia dawa za kuongeza nguvu michezoni.
Pogba, 30, alifanyiwa vipimo vya dawa aina ya DHEA Agosti mwaka jana, ambazo huongeza kiwango kikubwa cha homoni aina za testosterone.
Baada ya hapo alifungiwa kucheza soka kwa kosa hilo na kusababisha akae nje ya uwanja tangu Septemba mwaka jana.
Kwa mujibu wa gazeti la La Repubblica la Italia, upande wa mashtaka haukuamini madai ya Pogba ambaye alijitetea kwamba alikula dawa hizo bila ya kujua.
Akahukumiwa kifungo cha miaka minne cha kutojihusisha na soka ikidaiwa kuwa ni adhabu ya juu zaidi kuwahi kutolewa kwa mwanamichezo.
Kifungo chake kimehesabiwa kuanzia Septemba, 11, 2023 ambapo alifungiwa kwa muda wakati uchunguzi unaendelea na atakuwa huru Septemba, 10, 2027 ikiwa na maana kwamba staa huyu atarejea kwenye soka akiwa na umri wa miaka 34.
Hata hivyo, kwa mujibu wa tovuti ya SkySports Italia ni kwamba Pogba na wanasheria wake wamepanga kukata rufaa katika mahakama ya juu ya usuluhisi wa masuala ya michezo (CAS) huko Lausanne kupinga uamuzi huo.
Vilevile ripoti nyingine zimeeleza kwamba Pogba ambaye aliwahi kushinda Kombe la Dunia mwaka 2018 akiwa na Ufaransa anaweza kuamua kustaafu.
Pogba alitua Juventus kwa mara ya pili akitokea Man United mwaka 2022 na tangu hapo amekuwa akipitia nyakati ngumu za maisha yake ya soka akiandamwa na majeraha hadi kufikia kufungiwa.
Msimu uliopita alicheza mechi 10 za michuano yote na msimu huu amecheza mechi mbili tu.
Kabla ya kutua Juventus mwaka 2022, Pogba alihudumu Man United kwa miaka sita akiwa ndio mchezaji ghali zaidi kwenye timu hiyo baada ya kutua kwa ada ya uhamisho ya Pauni 89 milioni akitokea Juventus mwaka 2016..
Alicheza mechi 225 akiwa na Mashetani Wekundu hao akifunga mabao 39 na kutoa asisti 51.