Pigo Arsenal, Madueke aondoka kwa kuchechemea!
Muktasari:
- Baada ya tukio hilo, Madueke alibaki chini kwa muda na ikaonekana wazi hawezi kuendelea na mechi. Alitolewa dakika ya 60, akaenda benchi kabla ya kuingia moja kwa moja vyumbani kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imezidi kupata pigo kubwa la majeraha baada ya Noni Madueke kulazimika kutoka uwanjani katika mechi yao dhidi ya Sporting Lisbon.
Winga huyo wa kimataifa wa England alipata majeraha kutokana na mgongano mzito kati yake na Pedro Goncalves katika mechi ya mkondo wapili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyoisha kwa sare ya mabao 0-0, lakini Arsenal ilifuzu kwa jumla ya bao 1-0.
Baada ya tukio hilo, Madueke alibaki chini kwa muda na ikaonekana wazi hawezi kuendelea na mechi. Alitolewa dakika ya 60, akaenda benchi kabla ya kuingia moja kwa moja vyumbani kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.
Mshambuliaji chipukizi Max Dowman aliingia kuchukua nafasi yake na inaonekana huenda akapewa dakika zaidi iwapo Madueke atakuwa nje kwa muda.
Bado haijafahamika aina ya jeraha alilopata, ingawa inaonekana aliumia eneo la tumbo. Jeraha hili linakuja wiki chache tu baada ya kuumia akiwa na timu ya taifa ya England katika mechi ya kirafiki dhidi ya Uruguay na alitolewa nje pia.
Hali hii inaleta hofu kwa Arsenal, kwani ipo katika kipindi muhimu cha msimu, wakiwa wanapambania taji la Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa.
Katika mchezo huo, Arsenal pia ilikosa huduma za nyota kadhaa kutokana na majeraha, akiwemo Bukayo Saka, Martin Odegaard, Jurrien Timber na Riccardo Calafiori, ambao pia hawakuwepo katika kipigo dhidi ya Bournemouth mwishoni mwa wiki.
Kocha Mikel Arteta atahitaji kurejea kwa haraka kwa nyota wake muhimu, hasa kabla ya mechi dhidi ya Manchester City Jumapili ya wiki hii.