Tuchel akwepa mtego Arsenal
Muktasari:
- Tuchel ambaye ameiongoza England kufuzu kwa kishindo Kombe la Dunia kufuatia kushinda mechi zote nane, alisema: “Naelewa mtazamo wa watu. Lakini bado nina imani ya asilimia 100 na uaminifu wa Bukayo na Declan. Tumefanya vipimo vya kitabibu. Niliona hali zao. Declan hata wakati akitoka uwanjani hakuja kwangu na kusema ‘Narudi nyumbani’.”
LONDON, ENGLAND: HABARI ndio hiyo. Kocha wa England, Thomas Tuchel amefichua kuwa ruhusa aliyoitoa kwa mastaa wa Arsenal, wakiwemo Bukayo Saka na Declan Rice katika mechi ya kirafiki dhidi ya Japan haikuwa ‘danganya toto’ kama baadhi ya watu wanavyodhani, bali ni matokeo ya tathmini ya kitabibu.
Tuchel ambaye ameiongoza England kufuzu kwa kishindo Kombe la Dunia kufuatia kushinda mechi zote nane, alisema: “Naelewa mtazamo wa watu. Lakini bado nina imani ya asilimia 100 na uaminifu wa Bukayo na Declan. Tumefanya vipimo vya kitabibu. Niliona hali zao. Declan hata wakati akitoka uwanjani hakuja kwangu na kusema ‘Narudi nyumbani’.”
Kulingana na ripoti ya BBC, kati ya klabu 20 za Ligi Kuu England, wachezaji 228 waliteuliwa kuwakilisha nchi zao katika mechi za kimataifa. Hadi sasa, 23 kati yao wameondolewa na takriban nusu yao wakiwa wachezaji wa Arsenal.
Uondoaji huu unajitokeza wakati Arsenal wakishindania mataji matatu msimu huu, ikiwa ni pamoja na Ligi Kuu ya England, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa ya Ulaya.
Kabla ya wachezaji hao kuondolewa, Arsenal wameshuhudia mlolongo wa majeraha miongoni mwa wachezaji wao, ikiwemo kapteni Martin Odegaard, Gabriel, Jurrien Timber na Riccardo Calafiori.
William Saliba alikosa timu ya taifa ya Ufaransa kutokana na jeraha la kiwiko, huku Gabriel akiondolewa kwenye timu ya Brazil kwa shida ya goti.
Wachezaji wengine waliokosa kuungana na timu zao za taifa ni Eberechi Eze (mgongo wa kifundo cha mguu), Odegaard (goti), Jurrien Timber (misuli ya nyonga), na Leandro Trossard (kiuno).
Noni Madueke, Martin Zubimendi na Piero Hincapie pia waliondolewa kutokana na majeraha mbalimbali, wakichangia kuongezeka kwa changamoto ya majeraha kwenye washika mitutu hao wa London.
Kwa mujibu wa masharti ya FIFA yanataka wachezaji kuripoti kwa timu zao za taifa iwapo wateuliwa, ingawa timu za taifa zinaweza kufanya vipimo vya kitabibu ili kuthibitisha uwepo wa majeraha.
Tuchel alibainisha kuwa Saka na Rice walikuwa ‘wana hamu ya kucheza’ lakini kulikuwa na hatari ya kuongeza majeraha, hivyo kuwaondoa kwenye kikosi hicho ilikuwa ni kwa ushauri wa kitabibu.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amekabiliwa na changamoto hii mara kadhaa msimu huu, hasa wakati wachezaji wake wakubwa wanaposhindwa kuungana na timu zao za taifa.
Tuchel aliongeza uamuzi wa kuwaondoa wachezaji hao haukuwa rahisi kwake lakini ulifanyika kwa sababu ya kitaalamu, kuzingatia afya na usalama wa wachezaji hao.
Sakata hili linakumbusha maneno ya kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, aliyeona mechi za kirafiki za kimataifa kama “upotevu wa muda,” huku wachezaji wake wakikabiliwa na masharti makubwa kuachiwa.
Arsenal sasa inajiandaa kwa mechi ya Kombe la FA dhidi ya Southampton wikiendi ijayo na Ligi ya Mabingwa ya Ulaya dhidi ya Sporting Lisbon huku wakiwa na wachezaji wengi wenye historia ya majeraha.
Arsenal ni moja ya klabu zenye mafanikio makubwa zaidi katika soka England, ikiwa imebeba mara 13 ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo huku mara yao ya mwisho ikiwa msimu 2003–04 chini ya Arsene Wenger.
Pia inashilikia rekodi ya kuwa timu iliyobeba mara nyingi zaidi Kombe la FA (mara 14) huku ikiwa imeshinda Kombe la League Cup mara mbili na Ngao ya Jamii mara 16. Kwa upande wa michuano ya kimataifa ni washindi wa Inter‑Cities Fairs Cup mwaka 1970 na UEFA Cup Winners’ Cup mwaka 1994.