Piers Morgan amchana Arteta
Muktasari:
- Arsenal ilipoteza pointi muhimu Jumamosi iliyopita ilipokubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa West Ham United katika mechi ambayo ilipaswa kushinda ili kukimbizana na Liverpool kwenye mbio za ubingwa.
LONDON, ENGLAND: SHABIKI mnazi wa Arsenal, Piers Morgan amemshukia kocha wa timu hiyo Mikel Arteta juu ya uamuzi wake wa kuacha kusajili straika kwenye dirisha la Januari na kuigharimu timu hiyo ubingwa.
Arsenal ilipoteza pointi muhimu Jumamosi iliyopita ilipokubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa West Ham United katika mechi ambayo ilipaswa kushinda ili kukimbizana na Liverpool kwenye mbio za ubingwa.
Matokeo hayo yameifanya Arsenal kuwa kwenye wakati mgumu wa kutimiza ndoto za ubingwa baada ya sasa kuachwa nyuma kwa pointi 11 na Liverpool baada ya ushindi wao kwa Manchester City.
Mashabiki kadhaa wa Arsenal akiwamo Morgan, ambaye ni mshambulizi wamemshambulia Arteta kwa kushindwa kusajili straika mpya wakati alifahamu mapema kwamba Gabriel Jesus hatacheza hadi msimu ujao. Arsenal ilimpoteza straika mwingine, Kai Havertz wakati dirisha la usajili la Januari likiwa bado wazi, lakini kocha huyo Mhispaniola hakuangaika kusaka mshambuliaji mpya na sasa timu haina mtu kwenye fowadi.
Morgan alimtumia ujumbe Arteta aliosema: “Mpendwa Mikel Arteta…tunarudi nyuma tangu tuwe chini yako kwa kitendo chako cha kupuuzia kusajili mastraika wa kiwango cha dunia.”
Ujumbe huo wa Morgan aliuposti kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X na kuambatanisha picha ya mastraika wa Arsenal wa miaka ya karibuni.
“Kwa kukusaidia tu, tunahitaji washambuliaji wa kiwango kama hao. Mungu akisaidie utuletee mmoja.”
Arsenal ilitarajiwa kusajili straika mpya kwenye dirisha la Januari ili kuongeza nguvu kwenye safu yao ya ushambuliaji katika mbio za ubingwa na mmoja wa wachezaji iliyokuwa ikiwawinda ni Benjamin Sesko.
Lakini, alipuuza na kuamini Kai Havertz atasaidia timu hadi mwisho wa msimu, kabla ya fowadi huyo Mjerumani kuumia misuli ya nyuma ya paja akiwa na timu hiyo kwenye kambi ya mazoezi Dubai.