Penalti ya Silva yazua gumzo, Lunin afichua siri 

Muktasari:

  • Manchester City ya Pep Guardiola ilikuwa uwanjani kusaka ushindi wa aina yeyote ili kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa ilipowakaribisha mabingwa hao wa kihistoria wa michuano hiyo. Katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Madrid, Hispania uliisha kwa sare ya mabao 3-3. 

Kwa kawaida katika soka wadau, makocha na wachezaji wana usemi kuwa penalti huwa hazina mwenyewe. Ndivyo unavyoweza kuelezea kilichotokea usiku wa jana Jumatano kwenye Uwanja wa Etihad wakati Manchester City ikivuliwa taji la ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Real Madrid.


Manchester City ya Pep Guardiola ilikuwa uwanjani kusaka ushindi wa aina yeyote ili kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa ilipowakaribisha mabingwa hao wa kihistoria wa michuano hiyo. Katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Madrid, Hispania uliisha kwa sare ya mabao 3-3. 


Ikipewa nafasi kubwa kuibuka na ushindi kutokana aina ya soka lake, Manchester City ilitanguliwa kufungwa kwa bao la Rodrygo katika dakika ya 12 kabla ya Kelvin De Bruyne kurejesha bao hilo zikiwa zimesalia dakika 14 ya mchezo kumalizika. 


Katika dakika 30 za nyongeza wababe hao walishindwa kutambiana na mchezo kulazimika kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, ambapo Madrid imesonga mbele kwa kupata 4-3 za Man City. 
Katika mikwaju hiyo, Luka Modric ambaye alianza kupiga kwa upande wa Real Madrid alikosa baada ya kipa wa Manchester City, Ederson kucheza. Hata hivyo, mjadala mkubwa ni penalti ya kiungo mshambuliaji Bernardo Silva, ambaye mkwaju wake ulikwenda aliposimama kipa wa Madrid, Andriy Lunin. Mashabiki wa Man City na Guardiola mwenyewe walipigwa na butwaa huku ikiwa haifahamiki kama Silva alikuwa amepanga kupiga mkwaju huo kwa mtindo maarufu wa Panenka lakini ukashindikana.


Wachambuzi mbalimbali wameiponda penalti hiyo ambayo ilidakwa kirahisi na kipa Lunin ambaye pia aliudaka mkwaju wa Mateo Kovacic na kusema kuwa walijiandaa vizuri na mikwaju hiyo.


"Tulijiandaa vizuri kwa ajili ya mikwaju ya penalti tukiwa na kocha wetu, kuna wachezaji ambao tulishagudua kuwa watapiga na tulishasoma mienendo yao.


"Nafikiri mkwaju mwingine mmoja nilikuwa na uwezo wa kuudaka lakini nikafanya uzembe," alisema Lunin ambaye dakika chache kabla ya mikwaju ile alifanya mazungumzo na kipa msaidizi Kepa Arrizabalaga.